Tarehe 4 Desemba 2025, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa alifanya ziara ya kikazi jijini Osaka, ambapo alipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Profesa Takemura Keiko, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Osaka na Mhadhiri wa Kiswahili chuoni hapo. Mazungumzo yalilenga kuimarisha uhusiano wa elimu, lugha na diplomasia ya watu kwa watu kati ya Tanzania na Japan. Mheshimiwa Mutatembwa aliambatana na Bi. Edna Dioniz Chuku, Kansela wa Ubalozi. 

Mheshimiwa Mutatembwa alikishukuru Chuo Kikuu cha Osaka kwa kuendeleza na kuhimiza matumizi ya Lugha ya Kiswahili kupitia programu zake mbalimbali za lugha na utamaduni. Alisisitiza kuwa Tanzania inalitambua na kulithamini jukumu la kihistoria la chuo hicho katika kukuza na kuendeleza Kiswahili nchini Japan, lugha ambayo ni urithi na fahari ya Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla. Aidha, aliupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Osaka na kumpongeza Profesa Takemura kwa mchango mkubwa alioutoa katika kufundisha na kuendeleza utafiti kuhusu Kiswahili kwa takriban miongo minne.

Profesa Takemura, kwa upande wake, alieleza kuwa programu za Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Osaka zimeendelea kukua na kupokea wanafunzi wengi wa Kijapani, wanaovutiwa si tu na lugha, bali pia historia, utamaduni na maendeleo ya jamii za Afrika Mashariki. Alibainisha kuwa idara hiyo inapokea wanafunzi takriban themanini (80) kwa mwaka katika ngazi mbalimbali, ikiwemo shahada ya kwanza, shahada ya pili na uzamivu. Alieleza pia kuwa idara hiyo imekuwa ikifanya shughuli za kujenga umahiri wa Kiswahili, zikiwemo michuano ya kuigiza na mashindano ya hotuba ya Kiswahili yanayofanyika kila mwaka, ambayo huchochea ubunifu na uelewa wa lugha miongoni mwa wanafunzi.

Katika mazungumzo hayo, Profesa Takemura alielezea historia yake binafsi ya kusoma Kiswahili, akieleza kuwa aliamua kujifunza lugha hiyo kutokana na hamu yake ya kuelewa Afrika kwa undani zaidi, baada ya kugundua kuwa elimu kuhusu Bara hilo haikufundishwa kwa kina katika shule nyingi za Japan. Alibainisha kuwa hamu hiyo ilimfikisha Tanzania na Zanzibar mara kadhaa, ambapo alijifunza na kufanya utafiti wa Lahaja za Kiswahili, jambo lililomjengea umahiri na uelewa wa kipekee kuhusu lugha hiyo. Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Osaka na vyuo vya Tanzania, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), umeendelea kuleta matokeo chanya, ikiwemo mabadilishano ya wanafunzi na wahadhiri pamoja na tafiti za pamoja.

Mheshimiwa Mutatembwa alimhakikishia Profesa Takemura kuwa Ubalozi utaendelea kuunga mkono jitihada za chuo hicho, hususan katika kuratibu mawasiliano na taasisi za elimu nchini Tanzania ili kuimarisha zaidi ushirikiano huo. Pia, alieleza utayari wa Ubalozi kuhimiza mamlaka za Tanzania kushirikiana na Chuo Kikuu cha Osaka katika kuendeleza programu mpya, ikiwemo uwezekano wa kuanzishwa kwa masomo ya Kijapani katika vyuo vya Tanzania, programu za mafunzo ya ualimu na miradi ya tafiti za pamoja.

Mazungumzo hayo pia yalijadili changamoto za walimu wa kujitolea wa JICA ambao kabla ya janga la COVID-19 walikuwa wakifundisha Kiswahili Tanzania, na umuhimu wa kurejesha utaratibu huo au kuanzisha utaratibu mpya wa mafunzo endelevu kupitia ushirikiano wa kitaasisi. Profesa Takemura alitaja kwamba baadhi ya juhudi zimeanza kuwasilishwa na Chuo Kikuu cha Dodoma, ambacho kilieleza nia ya kuanzisha programu za Kijapani, jambo ambalo litaongeza fursa kwa wanafunzi na wataalamu kutoka pande zote mbili.

Mazungumzo yalihitimishwa kwa pande zote mbili kuthibitisha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa elimu kati ya Tanzania na Japan kupitia Chuo Kikuu cha Osaka. Mheshimiwa Balozi alialikwa kutembelea Kampasi ya Minoh katika Hafla ya Maadhimisho ya Miaka 40 ya Idara ya Kiswahili. Kwa upande wake, alishukuru kwa mwaliko huo na kuahidi kwamba Ubalozi utaendelea kushirikiana na chuo hicho; pamoja na kuhamasisha taasisi za elimu nchini Tanzania kushirikiana na Chuo Kikuu cha Osaka.
 

  • Mheshimiwa Anderson Mutatembwa kwenye picha na Profesa Takemura Keiko, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Osaka na Mhadhiri wa Kiswahili chuoni hapo, mara baada ya kuhitimisha mazungumzo.Mheshimiwa Anderson Mutatembwa kwenye picha na Profesa Takemura Keiko, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Osaka na Mhadhiri wa Kiswahili chuoni hapo, mara baada ya kuhitimisha mazungumzo.