Tarehe 30 Aprili 2026, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa University of Tsukuba, Dkt. Kyosuke Nagata. Chuo hicho kipo katika mji wa Tsukuba, Jimbo la Ibaraki, nchini Japan. Madhumuni ya ziara hiyo yalikuwa kujadili maeneo ya ushirikiano kati ya chuo hicho na vyuo vikuu vya Tanzania.
Aliongeza kuwa chuo hicho kina wanafunzi wa kimataifa 2,411 kutoka nchi mbalimbali, na kina ushirikiano na vyuo vikuu 383 katika nchi 67 pamoja na kuwa na ofisi 14 nje ya Japan. Kwa upande wa taaluma, chuo kina shule 11 zinazojumuisha fani mbalimbali, ikiwemo Humanities and Culture, Social and International Studies, Human Sciences, Life and Environmental Sciences, Science and Engineering, Informatics, Medicine and Health Sciences, pamoja na Arts and Design. Aidha, baadhi ya kozi zake hufundishwa kwa lugha ya Kiingereza, jambo linalorahisisha ushiriki wa wanafunzi wa kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Nagata alieleza utayari wa chuo hicho kuanzisha ushirikiano wa kitaaluma na vyuo vikuu vya Tanzania, hususan katika maeneo ya kubadilishana wanafunzi na wahadhiri, kufanya tafiti za pamoja pamoja na kuandaa makongamano ya kitaaluma. Alipendekeza kuwa ushirikiano huo uanze kwa programu za kubadilishana wanafunzi katika kozi ambazo tayari zinafundishwa katika chuo hicho.
Aidha, alieleza kuwa kuna fursa kubwa ya ushirikiano katika sekta ya michezo, ambapo chuo hicho kina umahiri mkubwa katika kutoa mafunzo ya taaluma mbalimbali za michezo.
Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa alimshukuru Dkt. Nagata kwa utayari huo na kueleza kuwa Ubalozi utachukua hatua za kuwasiliana na vyuo vikuu vya Tanzania ili viwasilishe mapendekezo ya programu za kubadilishana wanafunzi pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano.



