Tarehe 30 Aprili 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa, alifanya ziara kwenye Taasisi ya Utafiti wa Anga za Juu ya Japan, (Japan Aerospace Exploration Agency - JAXA). Lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya anga za juu, hususan katika utekelezaji wa mradi wa kurusha satelaiti ya kwanza ya Tanzania (TanzaniteSat-1). Mheshimiwa Balozi alipokelewa na viongozi wa JAXA wakiongozwa na Makamu wa Rais wa taasisi hiyo, Bw. ISHII Yasuo.
Pande zote zilijadili maendeleo ya Mradi wa Satelaiti ya Tanzania (TanzaniteSat-1); JAXA ikieleza kuwa inaendelea kushirikiana kwa karibu na timu ya Tanzania kupitia mikutano ya mara kwa mara ya kiufundi, na kubainisha kuwa uzinduzi wa satelaiti unatarajiwa kufanyika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ujao, kwa kutegemea ukamilishaji wa hatua za mwisho za maandalizi.
Makamu wa Rais wa JAXA alieleza historia na mafanikio ya Japan kwenye sekta ya anga za juu, pamoja na nafasi yao katika kuratibu na kutekeleza miradi ya sekta hiyo; na mchango wa JAXA katika kukuza ubunifu na ushirikiano wa kimataifa katika sekta hiyo. Aidha, alibainisha fursa mbalimbali za ushirikiano kwa nchi zinazoendelea kupitia Programu ya KiboCube, inayolenga kusaidia nchi zisizo na uwezo wa kurusha satelaiti kupata uzoefu wa vitendo katika teknolojia hiyo.
Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa alielezea dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na Japan katika teknolojia ya anga za juu na kufuatilia maendeleo ya Mradi wa TanzaniteSat-1. Alieleza kuwa mradi huo ni wa kimkakati kwa maendeleo ya Taifa, hususan katika ufuatiliaji wa mazingira na majanga, ukusanyaji wa taarifa kupitia earth observation, pamoja na kuimarisha sekta za kilimo, mawasiliano na usimamizi wa rasilimali. Aidha, alitoa rai kwa JAXA kuendelea kuwajengea uwezo wa wataalamu wa Tanzania kupitia mafunzo ya kisayansi na kiufundi.
Baada ya mazungumzo, Mheshimiwa Balozi alipata fursa ya kutembelea Kituo cha Anga cha Tsukuba, ambapo alijionea miundombinu ya kisasa ya uendeshaji wa Moduli ya Kibo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (International Space Station - ISS), maabara za majaribio ya satelaiti pamoja na maonesho ya teknolojia za anga za juu.





