Tarehe 29 Aprili 2026, Ubalozi ulipata fursa ya kutoa semina kuhusu Tanzania katika Tokyo University of Foreign Studies (TUFS), kupitia mpango wa utoaji wa semina katika vyuo vikuu mbalimbali unaoendeshwa na Mabalozi wa nchi za Southern African Development Community walioko nchini Japan, ujulikanao kama SADC Lecture Series.

Katika semina hiyo, Ubalozi uliwasilisha mada mbalimbali kuhusu Tanzania, ikiwemo jiografia na mahali ilipo, mfumo wa elimu, hali ya uchumi na sekta kuu zinazochangia uchumi, biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani ikiwemo Japan, vivutio vya utalii, pamoja na utamaduni wa vyakula na mavazi. Aidha, wasilisho liligusia pia masuala ya kisiasa na kijamii, pamoja na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Japan.

Baada ya wasilisho, wanafunzi wa chuo hicho, chini ya uratibu wa Profesa Sakai Makiko anayejihusisha na masuala ya kimataifa hususan Afrika, walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali. Maswali hayo yalihusu, miongoni mwa mengine, changamoto na mafanikio ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, maendeleo katika sekta ya elimu, pamoja na fursa za kujifunza zaidi kuhusu Tanzania. Wanafunzi walionyesha shauku kubwa ya kujifunza zaidi kuhusu Tanzania, hususan kupitia mafunzo ya lugha ya Kiswahili yanayotolewa chuoni hapo.

Mpango wa SADC Lecture Series umeendelea kwa muda mrefu, ukiwezesha vyuo vikuu mbalimbali nchini Japan kunufaika kwa kupata uelewa mpana kuhusu nchi za SADC. Ubalozi wa Tanzania umekuwa ukishiriki kikamilifu katika mpango huo kwa mujibu wa ratiba ya pamoja iliyopangwa na Mabalozi wa nchi za SADC, kwa lengo la kukuza uelewa wa kimataifa na kuimarisha mahusiano ya kirafiki kati ya Tanzania na Japan.