Tarehe 27 Februari 2026, Ubalozi ulitembelea Makao Makuu ya Taasisi ya Zimamoto ya Japan kwa lengo la kufanya mazungumzo kuishawishi Mamlaka hiyo kuendelea na mpango wake wa kutoa msaada wa magari ya zimamoto na uokozi kwa Tanzania; ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma yao ya kuisadia Tanzania kwa jumla ya magari 30 katika kipindi cha miaka mitano (2023–2028). Ubalozi uliwakilishwa na Bi. Edna Dioniz Chuku, Counsellor – Economic Affairs, Bw. Hosea Chikolongo, Mwambata Siasa na Utamaduni pamoja na Bi. Emi Tanaka, Katibu wa Balozi. 

Katika mazungumzo hayo, Mamlaka hiyo imekubali kuendelea kutoa msaada wa magari matano ya zimamoto na uokozi, na kushauri Ubalozi kuyapokea rasmi na kuomba Tanzania kukamilisha taratibu za usafirishaji wa magari hayo ili yasafirishwe nchini ifikapo mwezi Mei 2026. Mamlaka hiyo imeeleza kuwa endapo taratibu za usafirishaji zitakamilika kwa wakati, wanakusudia kuendelea na mpango wa kutoa msaada wa magari mengine katika kipindi cha Januari hadi Februari 2027; na magari yatakayosalia yanatarajiwa kutolewa kwa awamu mwaka 2027 na 2028, kulingana na upatikanaji na ratiba ya mpango husika.

Vilevile, Mamlaka hiyo ilishauri Tanzania kushirikiana na Japan kuanzisha programu maalum ya mafunzo kwa wataalamu wa zimamoto, hususan katika uendeshaji na matengenezo ya magari yatakayotolewa. Wameshauri maombi rasmi yawasilishwe Serikali ya Japan kupitia JICA ili kuwezesha uratibu wa mafunzo na kuwajengea uwezo wataalamu wa Tanzania (capacity building). Wakieleza kuwa wamekuwa wakitekeleza programu kama hizo katika nchi mbalimbali, ikiwemo za Afrika Mashariki, kwa kutuma wataalamu wao kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu kulingana na mahitaji ya nchi husika.