Tarehe 19 Februari 2026, Ubalozi ulifanya mkutano na wataalamu wa Tokushukai Medical Group pamoja na JGC Corporation kujadili maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupandikiza Figo unaotekelezwa kwa ubia kati ya Tokushukai na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mazungumzo hayo yalijikita katika tathmini ya hatua zilizofikiwa kufuatia ziara ya wataalamu wa Tokushukai na JGC (Consultant) iliyofanyika nchini Tanzania mwishoni mwa mwaka 2025, hususan katika mchakato wa ukamilishaji wa Grant Agreement kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati. Pande zote zilisisitiza umuhimu wa kuharakisha hatua za kisheria na kiutawala ili kuruhusu utekelezaji wa mradi kuanza kwa wakati uliopangwa.

Wataalamu hao walibainisha maandalizi yanayoendelea ya kufanya ziara nchini Tanzania mwanzoni mwa mwezi Machi 2026, ambapo inatarajiwa kukamilisha hatua za awali za usanifu wa kina (Detailed Design), kufanya tathmini ya kiufundi ya eneo la mradi, pamoja na kufanya majadiliano na wadau husika kuhusu ratiba ya utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake, Bi. Edna Dioniz Chuku, Counsellor - Economic Affairs, kwa niaba ya Ubalozi, aliwashukuru wataalamu hao kwa ushirikiano wao wa karibu katika kufanikisha maandalizi ya mradi huo. Alieleza kuwa Tanzania ina dhamira thabiti ya kuona mradi huo unatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa, kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha huduma za upandikizaji figo nchini na ukanda wa Afrika Mashariki. Aidha, alibainisha kuwa Ubalozi utaendelea kufuatilia kwa karibu hatua zote za maandalizi zinazoendelea kwa pande zote.