Tarehe 20 Februari 2026, Balozi Anderson Mutatembwa alitembelea Kampuni ya UCC (Ueshima Coffee Company) ya Japan na kufanya mazungumzo na Bw. Ryo Satomi, Afisa Mtendaji Mkuu (Sustainability Management) wa kampuni hiyo, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na UCC hususan katika zao la kahawa, ikiwemo kuongeza thamani, masoko na kuwawezesha wakulima wadogo. UCC ni miongoni mwa kampuni kubwa na kongwe za kahawa nchini Japan, yenye shughuli za uzalishaji, utafiti, ununuzi na usambazaji wa kahawa kutoka kwa wazalishaji mbalimbali wa kahawa duniani.
Katika mazungumzo, UCC waliwasilisha maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa ELPS (Enhanced Linkages between Private Sector and Small-scale Producers) unaowawezesha wakulima wadogo katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma kwa kutoa mafunzo ya kilimo bora, matumizi sahihi ya pembejeo na kuboresha mbinu za uchakataji wa awali wa kahawa. Aidha, ilibainishwa kuwa wamekuwa wakifanya ziara za mara kwa mara nchini kwa ajili ya ufuatiliaji na utoaji wa mafunzo kwa wakulima wadogo, ambapo mwezi Februari 2026 walifanya ziara yao ya sita tangu kuanza kwa utekelezaji wa Mradi huo mwaka 2024 (ikiwemo hatua za maandalizi zilizochukua takribani miaka miwili).
Vilevile, UCC walionesha nia ya kuongeza wigo wa ushirikiano na Tanzania katika masoko ya kahawa ya ubora wa juu (premium coffee); na kuendelea kuitangaza katika soko la Japan kwa kuandaa semina na maonesho ya kahawa ya Tanzania nchini Japan na kushirikisha vyombo vya habari na wadau wengine ili kuongeza uelewa na uhitaji wa kahawa ya Tanzania katika soko hilo.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa aliishukuru Kampuni ya UCC Ueshima Coffee Company kwa ushirikiano wake endelevu na Tanzania, hususan kupitia utekelezaji wa Mradi wa ELPS unaowawezesha wakulima wadogo kuongeza tija, ubora na kipato. Alieleza kuwa juhudi hizo zinachangia kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la kahawa na kukuza diplomasia ya uchumi kati ya Tanzania na Japan.
Aidha, alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uzalishaji na biashara ya kahawa, ikiwa ni pamoja na kuhimiza uzalishaji wa kahawa ya ubora wa juu (premium coffee) inayokidhi mahitaji ya soko la kimataifa. Alipongeza dhamira ya UCC ya kuendelea kuitangaza kahawa ya Tanzania nchini Japan kupitia semina, maonesho na majukwaa ya kibiashara, na kuahidi ushirikiano wa karibu wa Ubalozi katika kuratibu mawasiliano na wadau husika pamoja na kuhamasisha upatikanaji wa taarifa sahihi za uzalishaji na fursa za uwekezaji katika sekta ya kahawa nchini.




