Tarehe 20 Februari 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alitembelea Makao Makuu ya Japan Tobacco Inc. (JT) yaliyopo jijini Tokyo na kufanya mazungumzo na Bw. Masamichi Terabatake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo. Kampuni ya JT ni miongoni mwa kampuni kubwa kimataifa katika sekta ya tumbaku; na ni kampuni tanzu ya Tanzania Cigarette Company Plc (TCC Plc), ikiwa na umiliki wa hisa za ubia wa zaidi ya asilimia 75.

Bw. Terabatake alieleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi muhimu kwa JT katika upatikanaji wa malighafi (tobacco leaf) pamoja na utekelezaji wa shughuli za uzalishaji na biashara kupitia TCC Plc. Aidha, alibainisha dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania kupitia uwekezaji katika programu za maendeleo ya jamii, hususan katika maeneo yanayozalisha tumbaku. Alieleza pia utayari wa JT wa kuongeza kiwango cha uwekezaji katika programu hizo kwa kipindi cha mwaka 2026  – 2028, zikilenga maeneo manne makuu ambayo ni uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na vijana; miradi ya maji na afya; programu za elimu; pamoja na msaada kwa watu wenye ulemavu.

Balozi Mutatembwa alimshukuru Bw. Terabatake kwa ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya kampuni hiyo na Tanzania, hususan mchango wake katika utoaji wa ajira, mapato ya Serikali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii. Vilevile, alimhakikishia utayari wa Serikali ya Tanzania kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na JT. Aidha, alitumia fursa ya mazungumzo hayo kuiomba kampuni hiyo kuangalia uwezekano wa kuongeza wigo wa programu ya ufadhili wa masomo kwa Watanzania, ambayo kwa sasa hutoa ufadhili kwa mwanafunzi mmoja kwa kila awamu baada ya mhitimu kumaliza masomo yake.