Tarehe 7 Januari 2026, Mhe. Anderson Mutatembwa, amefanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), Dkt. Akihiko Tanaka, katika Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Tokyo.
Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Japan, ambao umejengeka kwa kipindi cha takribani miongo sita, hususan katika nyanja za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilibainisha dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano huo kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania pamoja na mikakati ya ushirikiano wa maendeleo ya JICA.
Aidha, walijadiliana kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea nchini Tanzania pamoja na fursa za kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano, ikiwemo katika sekta za kilimo, miundombinu, elimu, nishati, afya, rasilimali watu na maendeleo ya miji kupitia ushirikiano wa majiji pacha kwa nchi mbili (sister-city relations).



