Tarehe 8 Disemba 2025, Balozi Anderson Mutatembwa aliungana na Mabalozi wengine wa Nchi za Afrika (African Diplomatic Corps – ADC) katika Kikao cha tathmini ya Mkutano wa Tisa wa Kilele wa Maendeleo baina ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 9 Summit), kilichoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan. Waandaaji wenza wa TICAD, Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), walishiriki pia katika Kikao hicho.

Lengo kuu la Kikao hicho lilikuwa kufanya tathmini ya utekelezaji na maazimio ya TICAD 9 Summit, ambapo:

i) Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan, Balozi Takao Imafuku, aliwasilisha taarifa fupi kuhusu matokeo ya TICAD 9, ikijumuisha mafanikio yaliyopatikana pamoja na hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa maazimio ya mkutano huo;

ii) Waandaaji wenza wa TICAD, ambao ni Benki ya Dunia na UNDP, waliwasilisha taarifa kuhusu mchango wao katika maandalizi na utekelezaji wa TICAD 9, hususan katika maeneo ya ufadhili wa maendeleo, ujenzi wa uwezo, na uimarishaji wa ushirikiano wa kimkakati kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Bara la Afrika; na

iii) Amidi wa Mabalozi wa Afrika nchini Japan aliwasilisha salamu na kutoa shukrani kwa Serikali ya Japan kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Bara la Afrika.

Aidha, kikao kilijadili namna nchi za Afrika zinavyoweza kunufaika kikamilifu na fursa zilizotangazwa wakati wa TICAD 9. Fursa hizo zinahusisha maeneo kumi (10) yaliyojadiliwa na kukubaliwa wakati wa TICAD 9 uliofanyika mwezi Agosti 2025, jijini Yokohama, yakiwemo:
a) ujenzi wa uwezo kwa vijana 300,000 katika kipindi cha miaka mitatu (3);
b) mikopo na misaada ya maendeleo yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.5 kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), pamoja na dola za Marekani bilioni 5.5 kwa ajili ya kuwezesha sekta binafsi ya Japan kutekeleza programu na miradi mbalimbali barani Afrika; na
c) maeneo mengine manane (8) kama yalivyoainishwa katika Azimio la TICAD 9 Summit.

Kikao kilitoa fursa kwa Mabalozi kuwasilisha michango yao, ambapo ilikubalika kuwa utekelezaji wa maazimio ya TICAD 9 unahitaji ufuatiliaji wa karibu, uratibu wa pamoja, na mawasiliano ya mara kwa mara baina ya pande zote husika.