Tarehe 5 Machi 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alifanya ziara ya kikazi katika Kampuni ya Well Medical Group iliyopo jijini Tokyo, Japan, kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano katika sekta ya afya hususan katika teknolojia za tiba ya kisasa (regenerative medicine).
Katika ziara hiyo, Balozi Mutatembwa na ujumbe wake walipata wasilisho kuhusu shughuli za kampuni hiyo, ikiwemo matumizi ya teknolojia za stem cell therapy, uchunguzi wa afya (comprehensive health check-up), pamoja na mbinu za kisasa za kuzuia na kutibu magonjwa mbalimbali, ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza na yale yanayohusiana na uzee (anti-aging medicine).
Uongozi wa kampuni hiyo ulieleza kuwa tiba ya regenerative medicine ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi duniani, ikichochewa na maendeleo ya sayansi na teknolojia za matibabu. Walibainisha kuwa huduma wanazotoa zinajumuisha uchunguzi wa kina wa afya kwa kutumia vifaa vya kisasa kama MRI, CT scan na uchambuzi wa vinasaba (genetic analysis), sambamba na matibabu ya stem cell yanayolenga kurejesha na kuimarisha seli za mwili.
Aidha, kampuni hiyo ilieleza nia yake ya kupanua wigo wa huduma zake, ikiwemo uwezekano wa kuanzisha kituo cha tiba ya kisasa nchini Tanzania, hususan Zanzibar, ambacho kinaweza kuhudumia sio tu Tanzania bali pia nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo mengine ya Afrika. Ilielezwa kuwa mpango huo unaweza kujumuisha pia uanzishwaji wa kituo cha mafunzo kwa wataalamu wa afya katika teknolojia za regenerative medicine.
Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa aliishukuru kampuni hiyo kwa wasilisho na kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika sekta ya afya. Alieleza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kuwa kitovu cha huduma za afya za kisasa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na nafasi yake ya kijiografia na mahitaji makubwa ya huduma hizo. Aidha, alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji wa kimataifa katika kuendeleza sekta ya afya kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa na sera za uwekezaji. Alibainisha kuwa Ubalozi uko tayari kuratibu mawasiliano kati ya kampuni hiyo na mamlaka husika nchini, ikiwemo Wizara ya Afya na taasisi za uwekezaji, ili kuwezesha majadiliano na utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa pande zote.
Balozi Mutatembwa pia alitoa wito wa kuandaa Andiko dhana ya mradi (concept note) itakayowasilishwa rasmi kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya tathmini na hatua zaidi.




