Tarehe 2 Aprili 2026, Mhe. Anderson Mutatembwa, alimtembelea Mkuu wa Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa (UNU), Prof. Tshilidzi Marwala, kwenye Makao Makuu ya chuo hicho jijini Tokyo. Mazungumzo yao yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na UNU, hususan katika maeneo ya utafiti wa pamoja, maendeleo ya sera, na maendeleo endelevu.
Balozi Mutatembwa alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kitaaluma na taasisi za Tanzania pamoja na programu za kujengeana uwezo kwa wataalamu na watunga sera.
Kwa upande wake, Prof. Marwala alieleza utayari wa UNU kuendeleza ushirikiano huo kupitia tafiti, mafunzo, na uwezekano wa kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo (internships) kwa wanafunzi wa Kitanzania.
Pande zote mbili zilikubaliana kuimarisha mawasiliano kati ya UNU na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuweka utaratibu rasmi wa ushirikiano huo.
UNU ni taasisi ya kimataifa iliyoanzishwa mwaka 1973 kwa lengo la kufanya tafiti, mafunzo na kutoa ushauri wa kisera kuhusu changamoto za maendeleo duniani. Makao makuu yake yapo Tokyo, Japan.



