Tarehe 19 Februari 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alipokea Ujumbe wa wawakilishi kutoka ITO EN na Tully's Coffee Japan, ulioongozwa na Bw. Osamu Aizawa, Marketing Manager wa ITO EN, pamoja na Bw. Hirofumi Izumi, Head of Product Division wa Tully’s, katika Ofisi za Ubalozi, Tokyo.
Ujumbe huo ulifika Ubalozini kwa lengo la kujitambulisha na kuelezea shughuli wanazozifanya kwa kushirikiana na Tanzania, hususan katika biashara ya kahawa, ambapo kampuni hizo zimekuwa zikijihusisha na ununuzi na matumizi ya kahawa ya Tanzania kupitia mtandao wao wa biashara na kampuni tanzu ya Tully’s Coffee Japan.
Katika mazungumzo hayo, wawakilishi wa ITO EN na Tully’s walieleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakithamini ubora wa kahawa ya Tanzania, na wameendelea kuitumia katika baadhi ya bidhaa zao za vinywaji na kahawa kwa soko la Japan. Aidha, walibainisha kuwa wanatambua ongezeko la uhitaji wa kahawa yenye ubora na asili ya kipekee, na hivyo kuona Tanzania kuwa mshirika muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa kahawa yenye viwango vya kimataifa.
Waliongeza kuwa kampuni hizo zina nia ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wao na Tanzania kwa kupanua wigo wa ununuzi wa kahawa, kuendeleza uhusiano wa moja kwa moja na wadau wa sekta ya kahawa nchini, pamoja na kuchunguza fursa za kushirikiana katika uongezaji thamani, utangazaji wa kahawa ya Tanzania katika soko la Japan, na kuendeleza majukwaa ya kibiashara yanayowaunganisha wazalishaji na wanunuzi.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Mutatembwa aliwashukuru wawakilishi wa ITO EN na Tully’s kwa kuendelea kuamini ubora wa kahawa ya Tanzania na kwa mchango wao katika kukuza soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan. Aidha, aliwahakikishia ushirikiano wa Ubalozi katika kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya kampuni hizo na wadau wa sekta ya kahawa nchini Tanzania; pamoja na kuongeza juhudi za kuitangaza kahawa ya Tanzania katika soko la Japan ili kuongeza soko, ushindani na kipato kwa wakulima wadogo wa kahawa.



