Tarehe 19 Februari 2026, Balozi Anderson Mutatembwa alipokea Ujumbe wa wawakilishi wa Kampuni ya TERUMO ya Japan waliotembelea Ubalozi kwa lengo la kuendeleza majadiliano kuhusu ushirikiano wa sekta ya afya kati ya Tanzania na kampuni hiyo. Ujumbe huo uliongozwa na Bw. Tomokazu Kawase (Manager – Public and Private Partnership), akiambatana na timu yake inayoshughulikia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi pamoja na miradi ya kimkakati ya afya barani Afrika.

Katika mazungumzo yao, ujumbe wa TERUMO ulitoa shukrani zao kwa ushirikiano mzuri unaoendelea kati ya taasisi za Tanzania kupitia Wizara ya Afya na wadau wengine wa afya; katika majadiliano yanayoendelea ya ukamilishaji wa rasimu ya Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa na Terumo BCT Europe. Aidha, walisisitiza dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mfumo wa huduma za afya kupitia teknolojia za kisasa, uhamishaji wa ujuzi na mafunzo kwa wataalamu wa afya nchini.

Ujumbe huo ulitoa wasilisho kuhusu shughuli za Kampuni ya TERUMO kwa zaidi za mataifa160 duniani, ikiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 100 katika uzalishaji wa vifaa tiba, teknolojia za matibabu ya moyo na mishipa ya damu (cardiac and vascular care), teknolojia za damu (blood technologies), pamoja na suluhisho za mifumo ya tiba na ufuatiliaji wa wagonjwa. Ujumbe ulieleza ushirikiano wao na Tanzania kupitia maendeleo ya miradi inayohusiana na ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell Disease – SCD), ikiwemo matumizi ya teknolojia ya automated red blood cell exchange ambayo tayari imeanza kutumika katika baadhi ya hospitali kubwa nchini, ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa. Walibainisha kuwa hatua hiyo ni mafanikio makubwa kikanda, kwani Tanzania imepiga hatua mbele katika matumizi ya teknolojia za kisasa za tiba ya SCD ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Aidha, kampuni hiyo iliwasilisha mpango wake mpya wa kuongeza wigo wa ushirikiano na Tanzania kwa kuanzisha programu ya mafunzo ya matibabu ya moyo (cardiac catheterization and Percutaneous Coronary Intervention – PCI) kwa madaktari bingwa wa Tanzania, yenye lengo la kujenga uwezo wa kitaalamu katika matibabu ya magonjwa ya moyo hususan ischemic heart disease ambayo inaongezeka kwa kasi. Walieleza kuwa mafunzo hayo yanaweza kutolewa kupitia vituo vya simulation training nchini Japan, pamoja na uwezekano wa kuleta wataalam wa Japan kutoa mafunzo kwa vitendo nchini Tanzania.

Vilevile, TERUMO walieleza kuwa wamewasilisha pendekezo la ufadhili (grant proposal) kwa Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi wa Jamii ya Japan kwa ajili ya kuendeleza programu hiyo nchini Tanzania, na wanatarajia majibu mwishoni mwa mwezi Machi 2026. Wameshauri kuwa ushirikiano wa kisera na kitaasisi kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japan utakuwa muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, ikiwemo uwezekano wa kuwasilisha mahitaji rasmi ya Tanzania kupitia JICA.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa aliushukuru ujumbe wa Terumo Corporation kwa ushirikiano wao endelevu na mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini Tanzania, hususan katika matumizi ya teknolojia za kisasa za matibabu ya magonjwa ya damu na moyo. Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini ushirikiano wa kimkakati na kampuni hiyo pamoja na taasisi za afya za Japan katika kuendeleza huduma za afya zenye ubora na viwango vya kimataifa.

Aidha, alieleza kuwa hatua ya kuendelea na majadiliano ya ukamilishaji wa rasimu ya Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Serikali ya Tanzania na Terumo BCT Europe ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa huduma za afya, hususan katika maeneo ya teknolojia za damu na matibabu ya ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell Disease – SCD), ambao unaathiri sehemu kubwa ya jamii nchini. Alisisitiza kuwa mafanikio ya matumizi ya teknolojia ya automated red blood cell exchange katika hospitali za rufaa nchini, ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa, yanaonesha umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo wa kiteknolojia na kitaalamu.

Kuhusu mpango uliopendekezwa wa mafunzo ya matibabu ya moyo (cardiac catheterization na PCI), Mheshimiwa Balozi aliipongeza TERUMO kwa mpango huo wa kujenga uwezo wa wataalamu wa afya wa Tanzania, na kubainisha kuwa mpango huo unaendana na vipaumbele vya Serikali katika kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), hususan magonjwa ya moyo ambayo yanaongezeka kwa kasi. Alieleza utayari wa Ubalozi kuendelea kuratibu mawasiliano kati ya wadau wa Tanzania na taasisi za Japan, ikiwemo Japan International Cooperation Agency, ili kuwezesha utekelezaji wa programu za mafunzo, uhamishaji wa teknolojia na ubia wa kimkakati katika sekta ya afya.

Vilevile, Mheshimiwa Balozi aliipongeza kampuni hiyo kwa kuwasilisha pendekezo la ufadhili kwa Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi wa Jamii ya Japan, na kusisitiza kuwa ushirikiano wa kisera kati ya Serikali ya Tanzania na Japan utakuwa chachu muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa programu hizo. Aliwahakikishia ushirikiano wa karibu wa Ubalozi katika kufuatilia maendeleo ya pendekezo hilo, kuhamasisha uratibu wa kitaasisi na kuharakisha majadiliano ya MoU, kwa lengo la kuhakikisha miradi inayopendekezwa inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa ya muda mrefu kwa mfumo wa afya wa Tanzania na ukanda mzima.