Tarehe 29 Machi 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alikutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Wajapani waliojitolea nchini Tanzania (Japan Overseas Cooperation Volunteers - JOCV). Jumuiya hiyo inayojulikana, Waswahili No Kai, ilianzishwa mwaka 1986 kwa lengo la kuwakutanisha marafiki wa Tanzania waliopo Japan, hususan Wajapani waliowahi kuishi, kufanya kazi au kushiriki shughuli mbalimbali nchini Tanzania.

Waswahili No Kai ni jumuiya inayojumuisha wanachama wanaotoka katika nyanja mbalimbali, wakiwemo washiriki wa programu ya kujitolea ya Japan International Cooperation Agency (JICA) ijulikanayo kama Japan Overseas Cooperation Volunteers - JOCV, pamoja na wadau wa biashara, elimu, utamaduni na miradi ya maendeleo inayohusiana na Tanzania. Kundi hili lina wanachama takribani 400 na linaendelea kuwa daraja muhimu la kuimarisha urafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.

Kundi hili pia lina mchango mkubwa katika kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Kitanzania, kuwezesha kubadilishana uzoefu na maarifa, pamoja na kuunga mkono shughuli za maendeleo na ushirikiano wa kijamii kati ya mataifa haya mawili.

Akizungumza katika mkutano huo, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alitoa shukrani na pongezi za dhati kwa viongozi wa Waswahili No Kai kwa juhudi zao za kuanzisha na kuratibu kundi hilo muhimu. Alisisitiza kuwa kupitia uongozi wao mahiri, wamefanikiwa kuwaleta pamoja watu wenye mapenzi ya dhati kwa Tanzania na kuunda jukwaa lenye mchango mkubwa katika kuimarisha mahusiano ya watu kwa watu (people-to-people relations).

Aidha, aliwapongeza kwa kuendeleza ari ya kujitolea na ushirikiano unaochangia maendeleo ya Tanzania, akibainisha kuwa mchango wa Japan Overseas Cooperation Volunteers unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan na unastahili kuthaminiwa kwa kiwango cha juu.

Mwanzo na Mchango wa Wajitolea wa Kijapani (JOCV) nchini Tanzania

Programu ya Japan Overseas Cooperation Volunteers ilianza rasmi nchini Tanzania mwezi Machi 1967, ikiwa ni miongoni mwa makundi ya mwanzo kabisa kupelekwa barani Afrika. Tangu wakati huo, zaidi ya wajitolea 1,700 wamehudumu nchini Tanzania wakichangia katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, maendeleo ya jamii, ufundi stadi, michezo na maendeleo ya vijana.

Wajitolea hao wamehudumu katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania, ikiwemo:

Dar es Salaam (afya, TEHAMA na ufundi stadi),
Dodoma (maendeleo ya jamii na uwezeshaji wa wanawake),
Morogoro (miradi ya maendeleo ya jamii),
Ruvuma – Songea (kilimo),
Kilimanjaro – Moshi (kilimo na umwagiliaji),
Pwani – Bagamoyo (elimu ya wanawake na afya),
Mwanza - (elimu ya ufundi kupitia VETA),

Na mikoa mingine: Tanga, Iringa, Mbeya, Lindi, Mtwara na Zanzibar.

Kwa zaidi ya nusu karne, kupitia programu ya Japan Overseas Cooperation Volunteers, wajitolea wa Kijapani wameendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya Tanzania. Mchango wao umeacha alama ya kudumu katika jamii mbalimbali na kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa kirafiki kati ya Tanzania na Japan.