Tarehe 17 Februari 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alitembelea Makao Makuu ya Marubeni Corporation jijini Tokyo, na kufanya mazungumzo na watendaji wakuu wa kampuni hiyo wanaohusika na Idara ya Chakula na Biashara ya Mazao ya Kilimo.
Marubeni Corporation ni miongoni mwa kampuni kubwa za biashara nchini Japan (major Japanese general trading company) yenye ofisi katika takribani nchi 90 duniani, inayojishughulisha na biashara, uwekezaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo chakula, mazao ya kilimo, nishati, miundombinu na malighafi.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na kampuni hiyo, hususan katika biashara ya mazao ya kilimo. Mheshimiwa Balozi alitoa shukrani kwa ushiriki endelevu wa kampuni hiyo nchini Tanzania katika biashara ya kahawa, ufuta, viungo vya chakula na bidhaa nyingine, ambapo mchango wao umewezesha kupatikana kwa soko la bidhaa hizo nchini Japan na katika masoko mengine ya Asia. Alieleza kuwa ushirikiano wa Marubeni nchini umechangia pia kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo pamoja na uhamishaji wa maarifa kwa wakulima wadogo.
Kwa upande wao, uongozi wa Marubeni Corporation ulieleza kuwa kahawa ya Tanzania ni miongoni mwa bidhaa wanazozipa kipaumbele katika biashara yao ya chakula, na kwamba wanaendelea kushiriki katika miradi ya kuendeleza zao hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo. Wakitolea mfano, walieleza kuhusu Programu ya Enhanced Linkages between Private Sector and Small-scale Producers, inayolenga kuimarisha mnyororo wa thamani na kuwawezesha wakulima wadogo katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma. Aidha, walionesha nia ya kuendelea kuongeza wigo wa ushirikiano wa kibiashara na Tanzania katika uagizaji wa mazao mengine ikiwemo soya, viungo vya chakula (spices) na mahindi (corn), pamoja na kuomba taarifa zaidi kuhusu uwezo wa uzalishaji na upatikanaji wa bidhaa hizo kwa ajili ya soko la Japan.
Mheshimiwa Balozi Mutatembwa aliwahakikishia uongozi wa Marubeni Corporation kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kutoa wito kwao kuendelea kupanua wigo wa ushirikiano katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya kilimo, pamoja na kuahidi ushirikiano wa karibu wa Ubalozi katika kuratibu taarifa za uzalishaji, wadau husika na fursa za kibiashara zinazohitajika kwa soko la Japan.



