Tarehe 12 Machi 2026, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa alikutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Japan (Tanzania Students in Japan - TSJ).

Katika mazungumzo na Viongozi hao waliofika ubalozini kujitambulisha rasmi baada ya kuchaguliwa mwezi Desemba 2025 wakiongozwa na Mwenyekiti Bw. Fred Mkuyi walieleza mikakati waliyonayo katika kuimarisha Jumuiya hiyo ambayo ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama hai ambapo kwa sasa wapo 76 kati ya jumla ya Wanafunzi 143 wanaosoma Japan, kuendelea kutafuta fursa zaidi za ufadhili wa masomo kwa watanzania na kuwasaidia taratibu za kupata fursa hizo kupitia dawati la “Scholarship Help Desk”.

Katika mazungumzo yake, Balozi aliwashukuru kwa jitihada wanazozifanya kwa manufaa ya watanzania wengine kuendelea kupata fursa za masoma nchini Japan na kuwaahidi ushirikiano na ubalozi kuendelea kuzungumza na serikali ya Japan kuongeza fursa zaidi . Alieleza kuwa Japan ina fursa nyingi za ufadhili wa masomo mbali na zinazotambulika kupitia ubalozi wa Japan Tanzania ambazo ubalozi na Viongozi hao watashirikiana kuzitambua na kuona namna ya kuzipata na kuziwasilisha nyumbani ili wanaohitaji waweze kuomba.

Baadhi ya Viongozi wa Jumuiya hiyo walioambatana na Mwenyekiti ni Katibu Mkuu Bi. Queen Mshana, Naibu Katibu Bw. Deogratius Marwa, Mwenyekiti Kamati ya Katiba Bw. Maduhu Sengerema na Makamu Mwenyekiti Kamati ya Tekinolojia ya Habari Bw. Stephen Fungo.