Tarehe 25 Machi 2026, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa aliandaa mchapalo maalum kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Tokushukai Medical Corporation, Bw. Higashiue Shinichi, aliyembatana na wakurugenzi wa taasisi hiyo pamoja na jopo la madaktari kutoka Tanzania waliowasili nchini Japan kwa mwaliko wa taasisi hiyo.
Tokushukai Medical Corporation ina uhusiano wa muda mrefu na Tanzania katika sekta ya afya, hususan katika kubadilishana uzoefu, mafunzo ya kitaalamu na utoaji wa huduma za kibingwa. Aidha, taasisi hiyo imeonesha dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano huo kwa kushirikiana na Benjamin Mkapa Hospital (BMH) pamoja na University of Dodoma (UDOM) katika kuanzisha Kituo Bobezi cha Upandikizaji Figo na Viungo nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Balozi Mutatembwa alitoa pongezi kwa juhudi za Tokushukai Medical Corporation katika kuendeleza sekta ya afya nchini Tanzania, na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuboresha huduma za afya, hususan huduma za kibingwa. Alieleza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho kutachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama na changamoto zinazowakabili wagonjwa wanaohitaji huduma za upandikizaji figo nje ya nchi.
Kwa upande wake, Bw. Higashiue Shinichi alieleza utayari wa taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya afya, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya wataalamu, utafiti na uboreshaji wa miundombinu ya huduma za afya.
Hafla hiyo ilitoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu na kujadili njia bora za kuimarisha ushirikiano uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.



