Tarehe 12 Machi 2026, Balozi Anderson Mutatembwa alitembelea Makao Makuu ya Sekretarieti ya Japan International Association for the Industry of Urban Development, Building and Housing (JUBH) na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wake, Bw. Hiroto Izumi, ambaye pia alikuwa Mshauri Mkuu wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Japan, Hayati Shinzo Abe.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na makampuni ya Japan katika sekta ya maendeleo ya nyumba na makazi, hususan katika maeneo ya uwekezaji wa ujenzi wa makazi ya gharama nafuu, upangaji na uendelezaji wa miji, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa na endelevu katika ujenzi. Aidha, pande zote zilijadili fursa zilizopo nchini kutokana na ongezeko la mahitaji ya makazi na kasi ya ukuaji wa miji, pamoja na namna makampuni ya Japan yanavyoweza kushiriki katika miradi hiyo kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) na uwekezaji wa moja kwa moja.
Kwa upande wa Japan, ilielezwa wazi nia ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na Tanzania, ikitambuliwa kuwa Tanzania ni moja ya masoko yenye fursa kubwa za uwekezaji barani Afrika, hususan katika sekta ya makazi na maendeleo ya miji. Ilibainishwa kuwa, kutokana na kasi ya ukuaji wa miji na ongezeko la idadi ya watu, Tanzania ina uhitaji mkubwa wa nyumba unaokadiriwa kufikia takribani milioni tatu, hali inayotoa fursa pana kwa wawekezaji wa ndani na nje kushiriki katika ujenzi wa makazi, ikiwemo makampuni ya Japan.
Vilevile, ilibainishwa kuwa uzoefu na teknolojia ya Japan katika ujenzi wa makazi bora, ya gharama nafuu na rafiki kwa mazingira, unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukidhi mahitaji hayo nchini. Kwa muktadha huo, makampuni ya Japan yalihamasishwa kuendelea kuchangamkia fursa zilizopo nchini, ikiwemo uwekezaji katika miradi ya nyumba za gharama nafuu, maendeleo ya miji mipya, pamoja na kuimarisha ushirikiano na sekta ya umma na binafsi nchini.
Ubalozi utaendelea kutoa hamasa kwa makampuni hayo kutoka Japan katika kukuza maendeleo ya sekta hiyo muhimu ya nyumba na makazi nchini, ili kuwezesha utekelezaji wa ushirikiano uliokusudiwa, kufuatia ziara yao iliyofanyika nchini mwezi Julai 2025.



