Tarehe 9 Februari 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa, alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Nippon, Bw. Yohei Sasakawa. Taasisi ya Nippon ilianzishwa mwaka 1962 na inajihusisha na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo afya, hususan mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukoma, elimu kupitia ufadhili wa masomo, pamoja na maendeleo ya jamii.
Taasisi hiyo pia inatekeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira, hususan katika maeneo ya bahari, uhamasishaji wa kilimo chenye tija kwa wakulima wadogo, pamoja na uendelezaji wa amani. Katika mazungumzo hayo, Balozi Mutatembwa alimpongeza Bw. Sasakawa kwa mchango wake mkubwa katika kuhudumia jamii na kuhamasisha maendeleo endelevu, hususan katika sekta ya kilimo na uchumi wa buluu, na aliomba Taasisi hiyo kuangalia maeneo ambayo inaweza kushirikiana na Tanzania.
Kwa upande wake, Bw. Sasakawa alieleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na programu za kujenga uwezo kwa wataalamu katika masuala ya bahari, na kwamba Taasisi ya Nippon itafanya tathmini ya kubaini maeneo mengine zaidi ya ushirikiano na Tanzania. Aidha, alieleza kuwa mwaka 2024, akiwa na umri wa miaka 85, alipanda Mlima Kilimanjaro na kusimika ujumbe kuhusu kutokomeza ugonjwa wa ukoma na kupinga unyanyapaa dhidi ya waathirika wa ugonjwa huo, kama sehemu ya juhudi za kuhamasisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo. Aliongeza kuwa moja ya malengo yake ilikuwa ni kuvunja rekodi ya dunia ya mtu mwenye umri mkubwa zaidi kupanda mlima huo, na kwamba anatarajia kupanda tena Mlima Kilimanjaro mwaka 2027 akiwa na umri wa miaka 88 ili kutimiza lengo hilo.
Vilevile, Bw. Sasakawa alieleza kuwa Taasisi ya Nippon inatarajia kuitisha Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Afya wa Bara la Afrika utakaofanyika mnamo mwezi Juni 2026, Addis Ababa, Ethiopia, kwa lengo la kujadili jitihada za kutokomeza ugonjwa wa ukoma; ambapo, aliomba ushiriki wa Tanzania kwa ngazi husika. Aliongeza kuwa mwaka 2025 Taasisi hiyo iliandaa Mkutano wa Watu wenye Ushawishi kuhusu masuala ya Ustawi wa Jamii, ambapo kwa upande wa Tanzania alishiriki Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Alieleza kuwa mikutano hiyo itaendelea kufanyika kila mwaka, huku Tanzania ikiombwa kushiriki katika Mkutano utakaopangwa mwaka 2026.
Balozi Mutatembwa aliipongeza Taasisi ya Nippon kwa mchango wake mkubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukoma na juhudi za kuimarisha ustawi wa jamii, hususan barani Afrika. Aidha, aliihakikishia Taasisi hiyo kuwa Ubalozi utawasilisha taarifa ya Tanzania ya kushiriki katika Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Afya wa Bara la Afrika unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni 2026, Addis Ababa, Ethiopia, na katika mikutano mingine itakayofanyika chini ya uratibu wa Taasisi ya Nippon, kwa kuwa inaendana kikamilifu na vipaumbele vya nchi.
Vilevile, Balozi Mutatembwa alisisitiza dhamira ya Ubalozi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na Taasisi ya Nippon katika maeneo ya afya, hususan kutokomeza ugonjwa wa ukoma, pamoja na sekta za kilimo, uchumi wa buluu, na maendeleo ya jamii kwa ujumla.



