Tarehe 10 Februari 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa, alikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Ito Hiroyuki, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Wizara ya Sheria ya Japan, katika Ofisi za Idara hiyo zilizopo Tokyo.
Lengo kuu la mazungumzo hayo lilikuwa ni kujitambulisha rasmi pamoja na kutoa shukrani kwa Wizara ya Sheria ya Japan kufuatia kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano (MoC) kati ya Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Sheria ya Japan mnamo mwezi Agosti, 2025 pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 9, jijini Yokohama, Japan.
Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Balozi alieleza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ya Tanzania imeshakamilisha maandalizi ya Mpango Kazi wa Ushirikiano, ambao unatarajiwa kujadiliwa kwa pamoja wakati wa ziara rasmi ya Ujumbe kutoka Wizara ya Sheria ya Japan itakayofanyika nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Bw. Ito Hiroyuki alieleza kuwa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Wizara ya Sheria ya Japan ina ushirikiano wa kisheria na jumla ya nchi 14, ambapo kwa Bara la Afrika, Tanzania ndiyo nchi pekee inayonufaika na ushirikiano huo. Alibainisha kuwa hali hiyo inaonesha umuhimu mkubwa unaotolewa na Serikali ya Japan katika kuimarisha uhusiano wa kisheria na Tanzania. Aidha, taarifa ilitolewa ya mpango wa Wizara hiyo kutembelea Tanzania ifikapo mwezi Aprili kwa ajili ya majadiliano na Timu ya Watalamu wa Tanzania kuhusu utekelezaji wa MoC husika.



