Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akifuatilia Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa TICAD (siku ya kwanza) katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres Tunis, Tunisia, 27 Agosti 2022.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, akizungumza na Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida (hayupo pichani) kwa njia ya mtandao kwenye ukumbi wa Palais des Congres, Tunis, Tunisia tarehe 27 Agosti 2022.
Waziri Mkuu Khasim Majaliwa, kwenye picha ya pamoja na Bw. Tetsuro Yano, Rais wa Association of Africa Economy and Development (AFRECO) kabla ya mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 8, tarehe 27 Agosti 2022
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akifuatilia Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa TICAD (kwa siku ya pili) katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres Tunis, Tunisia, 28 Agosti 2022.
Waziri Mkuu Khasim Majaliwa, kwenye picha ya pamoja na Bw. Mutsuo Iwai, Mwenyekiti wa Bodi ya Japan Tobacco Inc. (JT Group) kabla ya mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 8, tarehe 28 Agosti 2022
Waziri Mkuu Khasim Majaliwa, kwenye picha ya pamoja na Bw. Yasuteru Hirai, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mitsubishi, kabla ya mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 8, tarehe 28 Agosti 2022
Waziri Mkuu Khasim Majaliwa, kwenye picha ya pamoja na Dkt. Tanaka Akihiko, Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kabla ya mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 8, tarehe 29 Agosti 2022
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa Majaliwa, akizungumza na Waziri Mkuu wa Tunisia Mhe. Najla Bouden Romdhane mara baada ya kupokelewa katika uwanja wa ndege wa Carthage, jijini Tunis tarehe 26 Agosti 2022.
Waziri Mkuu Khasim Majaliwa, akiwa kwenye mazungumzo na Bw. Tetsuro Yano, Rais wa Association of Africa Economy and Development (AFRECO), tarehe 27 Agosti 2022, pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 8
Waziri Mkuu Khasim Majaliwa, akiwa kwenye mazungumzo na Dkt. Tanaka Akihiko, Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), tarehe 29 Agosti 2022, pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 8
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Macky Sall pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 8 mjini Tunis, Tunisia

Mkutano wa Nane wa Kilele wa TICAD (Eighth Summit of Tokyo International Conference on African Development – TICAD 8) ulifanyika tarehe 28 – 29 Agosti 2022 mjini Tunis nchini Tunisia;  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliwakilishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) katika Mkutano huo. 

Hii ni mara ya pili kwa Mkutano huo kufanyika kwenye Bara la Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 baada ya ule uliofanyika nchini Kenya mwaka 2016 (TICAD 6). Aidha, Mkutano huo ulitanguliwa na Kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika nchini Japan, kilichofanyika tarehe 25 Agosti 2022. 

Mkutano wa TICAD 8 uliandaliwa na Serikali za Tunisia na Japan kwa kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo wakiwemo Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP); na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000 kutoka katika nchi 55 za Bara la Afrika na mashirika mbalimbali ya Kimataifa zikiwemo sekta binafsi hususan, wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Japan na Afrika kwa ujumla. Kauli mbiu ya Mkutano huo ilikuwa “Kukuza Maendeleo Endelevu ya Afrika kwa ajili ya Waafrika” (Promoting Africa-led, African-owned Sustainable Development).

Hotuba fupi zilitolewa na viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika, Serikali ya Japan pamoja na watendaji wakuu wa taasisi na maashirika ya maendeleo, ikiwa ni mojawapo ya sehemu za ufunguzi wa mkutano huo. Waziri Mkuu, Mhe Khassim Majaliwa alitumia nafasi hiyo kutoa Hotuba ya Tanzania iliyolenga hali ya uchumi duniani  kwa sasa jinsi ilivyoathiriwa na UVIKO 19 pamoja vita ya Ukraini na Urusi ambavyo imepelekea kupanda kwa bei za bidhaa na uhaba wa chakula. Mada ya hotuba hiyo ilihusu “Achieving Sustainable and Inclusive Growth with Reduced Economic Inequalities”. Kupitia hotuba hiyo, alielezea mikakati mbalimbali ambayo Serikali ya Tanzania inatekeleza ili kujikwamua kwenye hali ya mtikisiko wa kiuchumi duniani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa inashirikiana na sekta ya viwanda kushughulikia changamoto za kitaasisi katika utoaji wa huduma, kukuza uwekezaji na biashara na kukuza maendeleo ya wananchi wake.

Mkutano wa TICAD 8 ulijadili na kukubaliana namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063). Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika.

Pamoja na masuala mengine yaliyojiri kwenye Mkutano wa TICAD 8, Serikali ya Japan kupitia Hotuba iliyotolewa na Mhe. Fumio Kishida, Waziri Mkuu wa Japan wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, imeahidi kutoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 30 kwa kipindi cha miaka mitatu (2022 – 2025) kwa nchi za Bara la Afrika ili kuziwezesha kutekeleza programu na miradi ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi kwenye nchi hizo. 

Aidha, Serikali ya Japan imezihakikishia nchi za Afrika kuwa itaendeleza ushirikiano wa karibu kwa kuchangia maendeleo kupitia programu na miradi mbalimbali; na pia kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na changamoto zinazokwamisha juhudi za Afrika za kujikwamua kiuchumi kama vile milipuko ya magonjwa, mabadiliko ya tabia nchi na upungufu wa chakula. Serikali ya Japan imetangaza kutenga Yen bilioni 10 sawa na dola za Marekani milioni 70 kwenye mfuko wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika ujulikanao Comprehensive Africa Agriculture Development Program (CAADP) ili kukabiliana na baa la njaa barani Afrika. Kwa kupitia mpango huo, Serikali ya Japan imeahidi kutoa dola za Marekani laki 5 (500,000) kwa Tanzania kwa ajili ya kuboresha miradi ya kilimo kwa lengo la kukabiliana na baa la njaa nchini kufuatia athari za UVIKO – 19 na mgogoro wa kivita unaoendelea kati ya Urusi na Ukraini. 

Pia, Tanzania imeteuliwa na Shirika la JICA kuwa nchi ya mfano miongoni mwa nchi za Afrika (a model country) katika mpango wake wa kuimarisha kilimo cha uzalishaji wa mpunga barani Afrika, kutokana na kuwa mpango huo unatekelezwa nchini Tanzania kwa mafanikio makubwa. 

Vilevile, katika Mkutano wa TICAD 8, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweza pia kuwasilisha miradi nane (08) ya kipaumbele iliyojikita kwenye sekta za miundombinu, nishati, kilimo, maji, mifugo, uvuvi na uchumi wa buluu kwa ajili ya kuzingatiwa na Serikali ya Japan kuipatia ufadhili ili kuwezesha utekelezaji wake. Miradi hiyo nane iliyowasilishwa ni ya kipaumbele kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.334, ambayo ni: Mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa Barabara ya Morogoro hadi Dodoma  kwa kiwango cha rami yenye urefu wa km 260; Mradi wa Uendelezaji wa Umwagiliaji na Usimamizi wa Vyanzo vya maji katika Bonde la Ziwa Victoria (Irrigation Development and Watershed Management Project in the Lake Victoria Basin - IDWaMP); Mradi wa Usambazaji wa Maji wa Lugoda uliopo Wilaya ya Mufundi, Mkoani Iringa; Kuimarisha uwezo wa kufanya utafiti wa uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji, Tanzania  (Strengthening Fisheries and Acquaculture Research Capacity in Tanzania); Mradi wa Ujenzi wa bandari nne za kisasa za uvuvi, Zanzibar; Uanzishwaji wa maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi, Zanzibar;  Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Bandari ya Wete; na Mradi wa Usafirishaji Umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Somanga Fungu hadi Mkuranga.

Kadhalika, katika mkutano huo Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipata fursa ya kufanya mazungumzo ya pembezoni na Waziri Mkuu wa Tunisia, Mhe. Najla Bouden; Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Fumio Kishida; pamoja na baadhi ya watendaji wakuu wa kampuni na taasisi za Japan ikiwemo Shirika la Maendeleo la Japan (JICA); Kampuni ya Mitsubishi; Bodi ya Japan Tobacco Inc (JT Group); na Taasisi ya Japan inayojishughulisha na Uchumi na Maendeleo ya Afrika (Association of African Economy and Development -  AFRECO).  Mazungumzo hayo yalilenga mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania pamoja na yale ya kibiashara, kisiasa na kidiplomasia. 

Tangu kuanza kwa mikutano ya TICAD, Japan imekuwa ikiongeza kiasi cha fedha za mkopo wa masharti nafuu na msaada katika kuchangia maendeleo ya Afrika kutoka Dola za Marekani bilioni 0.6 kwa mwaka 1993 (TICAD 1) hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 20 kwa mwaka 2019 (TICAD 7). Kwa upande wa Tanzania misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka Japan imesaidia katika utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, afya, nishati ya umeme, kilimo na elimu. Tanzania ni nchi pekee inayoshirikiana na Japan katika maeneo matatu ya ushirikiano yaliyopewa kipaumbele na nchi hiyo ikiwemo, ushirikiano katika misaada na mikopo ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo; ujuzi na uzoefu kupitia program ya wajapani ya kujitolea chini ya Japan Overseas Cooperation Agreement; na fursa za mafunzo na masomo.