Tarehe 26 Aprili 2026, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan uliadhimisha miaka 62 ya Muungano kwa kuandaa mashindano ya mpira wa miguu yajulikanayo, MUUNGANO CUP, yaliyoshirikisha jumla ya timu 15.
Mashindano hayo yalihusisha timu mbalimbali zikiwemo Kilimanjaro Football Club na Zanzibar Heroes, pamoja na timu kutoka nchi za Kenya, Uganda, Burkina Faso, Nigeria, Senegal, Cape Verde, Vietnam, Malawi na Sri Lanka. Katika mashindano hayo, timu kutoka Senegal iliibuka mshindi, huku Kilimanjaro Football Club ikishika nafasi ya nne.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, alielezea umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya, kukuza mshikamano, na kuimarisha urafiki miongoni mwa mataifa mbalimbali. Aidha, alisisitiza kuwa michezo ni chombo muhimu cha kuzitangaza nchi zetu kimataifa, pamoja na kuendeleza diplomasia ya watu kwa watu.
Balozi Mutatembwa aliongeza kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya kuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, huku yakitumika pia kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka mataifa tofauti wanaoishi nchini Japan katika mazingira ya urafiki na ushirikiano.





