Tarehe 27 Aprili 2026, Ubalozi ulipokea ujumbe kutoka Children Meet Countries (CMC) yenye makao makuu jijini Tokyo. Taasisi hiyo imekuwa ikiandaa warsha na semina maalum mashuleni kwa lengo la kuwapa wanafunzi wa Japan uelewa kuhusu masuala ya kimataifa na tamaduni za nchi mbalimbali.

Akipokea ujumbe huo kwa niaba ya Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa, Bi. Edna Dioniz Chuku, Mshauri wa Masuala ya Uchumi wa Ubalozi (Counselor Economic Affairs), aliipongeza taasisi ya CMC kwa jitihada zake za kuelimisha vijana kuhusu umuhimu wa uelewa wa kimataifa. Aidha, alieleza utayari wa Ubalozi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kuandaa programu zitakazosaidia kuitangaza Tanzania, hususan katika maeneo ya utalii, utamaduni, elimu na fursa za biashara kwa bidhaa za Tanzania nchini Japan.

Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilikubaliana kuendelea kushirikiana katika kuandaa warsha na semina zitakazohusisha wanafunzi wa Japan, kwa kuzingatia mada mbalimbali zinazohusu Tanzania, ikiwemo historia, utamaduni, lugha ya Kiswahili pamoja na vivutio vya utalii. Lengo ni kuongeza uelewa na kukuza uhusiano wa kirafiki kati ya Tanzania na Japan.