Tarehe 25/04/2026 Balozi Anderson Mutatembwa alifungua maonesho ya 17 ya Tingatinga ya Kampuni ya Baraka ambayo hufanyika kila mwaka katika ukumbi wa Gallery Paris Jijini Yokohama nchini Japan.
Katika hotuba ya ufunguzi huo, Balozi Mutatembwa alitoa shukurani zake kwa wamiliki wa kampuni hiyo kwa kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania na utamaduni wake. Alielezea vivutio vingi vya utalii vilivyopo nchini Tanzania na kuwashawishi watembelee na kujionea wenyewe.
Maonesho hayo ambayo hufanyika kwa siku 10, hukutanisha watu mbalimbali akiwemo Bw. Shinichi Goto aliyewahi kuwa Balozi wa Japan nchini Tanzania. Katika maonesho hayo pia, huhusisha uuzaji wa vitu vya utamaduni wa Tanzania vikiwemo michoro ya Tingatinga, Kanga, Vitenge, mashuka ya kimasai na vitu vya Urembo. Pia, huuza Kahawa na Korosho za Tanzania.
Kampuni ya Baraka inamilikiwa na Bw na Bibi. Shimaoka raia wa Japan wanaoishi Zanzibar kwa miaka zaidi ya 35 sasa.




