Ikulu ya Kifalme, Tokyo.
Tarehe 28 Aprili 2026, Mheshimiwa Anderson Gukwi Mutatembwa, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, aliwasilisha Hati za Utambulisho (Letter of Credence) kwa Mfalme wa Japan, Naruhito, katika hafla ya kifalme iliyofanyika Ikulu ya Kifalme jijini Tokyo. Aidha, aliwasilisha Hati za Wito (Letter of Recall) za Balozi Baraka Luvanda aliyemaliza muda wake mwezi Agosti 2025.
Katika hafla hiyo, Mheshimiwa Balozi alipokelewa na Afisa Mkuu wa Shughuli za Kifalme (Grand Master of Ceremonies), Bw. Miyazawa na baadaye kupata fursa ya mazungumzo na Waziri wa Fedha wa Japan, Bi. Satsuki Katayama, kabla ya kuwasilisha Hati kwa Mfalme. Katika mazungumzo hayo, alielezea umuhimu wa uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan uliodumu kwa zaidi ya miaka 60 na mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, wakati wa uwasilishaji wa Hati za Utambulisho, Balozi Mutatembwa aliwasilisha salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Mfalme Naruhito. Aidha, alieleza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya pande zote.
Kwa upande wake, Mfalme Naruhito alituma salamu za heri na afya njema kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuelezea kufurahishwa kwake na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Japan. Alibainisha kuwa ingawa hajawahi kutembelea Tanzania, anatambua uwepo wa vivutio vya kipekee vya utalii pamoja na utajiri wa utamaduni uliopo nchini. Vilevile, alieleza kumbukumbu nzuri aliyonayo alipokuwa na umri wa miaka 20, kabla ya kuwa Mfalme, alipata fursa ya kumuona Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati wa ziara yake ya Kitaifa nchini Japan mwaka 1985. Alimpongeza Mheshimiwa Balozi na kumtakia mafanikio mema katika utekelezaji wa majukumu yake, akieleza imani yake kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Japan utaendelea kuimarika.
Balozi Mutatembwa alitoa shukrani za dhati kwa Serikali na wananchi wa Japan kwa ushirikiano mzuri uliopo, na kubainisha kuwa Tanzania inaitambua Japan kama mshirika wa karibu na muhimu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN
TOKYO





