Tarehe 2 Julai 2024, Ubalozi ulitembelewa na Ujumbe wa Kampuni ya Watarai Electrical Construction, miongoni mwa kampuni za Watarai Group yenye Makao Makuu Yamagata Japan, inayojishughulisha na masuala ya mazingira, maji na nishati ya umeme. Ujumbe huo uliongozwa na Bw. Masahiko Tanji, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, aliyeambatana na Bi. Fukuyo Nakamori, Mwenyekiti wa Taasisi ya Asia Pacific Africa (APA) Association, waandaaji wa Kongamano la Kuwezesha Wanawake Kiuchumi wa Nchi za Asia, Pasifiki na Afrika (APA Women's Economic Exchange Forum).

Bw. Tanji alieleza shabaha ya ujio wao ni kutoa taarifa kuhusu ziara inayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania na kampuni hiyo, mnamo tarehe 12 – 23 Julai 2024 (awamu ya kwanza) na mwezi Septemba 2024 (awamu ya pili, kwa tarehe zitakazopangwa baadaye). Alieleza kuwa kampuni yake imepewa dhamana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kufanya upembuzi (feasibility survey) kwenye masuala ya umeme, mazingira na maji kwa nchi zinazoendelea.

Aidha, alibainisha kuwa kwa awamu ya kwanza, timu ya wataalam watatu (03) wa kampuni hiyo inatarajiwa kuitembelea Tanzania kwa ajili ya kukusanya taarifa (feasibility survey) na kuwa na mazungumzo ya awali na taasisi zinazohusika na masuala ya maji ikiwemo, Wizara ya Maji. Pia, timu hiyo ingependelea kuitembelea shule mojawapo ya msingi iliyopo Dodoma kwa ajili ya mazungumzo ya uwezekano wa kutoa misaada ya kuwezesha upatikanaji wa maji shuleni hapo. Alieleza kuwa, katika awamu ya pili anatarajia kuongoza Ujumbe wa kampuni hiyo wenye wataalam nane (08) kuitembelea Tanzania mnamo mwezi Septemba 2024. 

Ziara hii, ni miongoni mwa matokeo ya makubaliano ya Kongamano la Kwanza la Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi lililofanyika mjini Tokyo mwezi Novemba 2022 na kuhudhuriwa na Mhe. Mama Mary Majaliwa. Katika Kongamano hilo, pamoja na mambo mengine, masuala ya upatikanaji wa maji safi na salama mashuleni na katika jamii za vijijini yalijadiliwa.