Tarehe 7 Februari 2023, Balozi Baraka Luvanda alikutana na kufanya mazungumzo na kundi la wafanyabiashara na wawekezaji wa New Zealand jijini Auckland, New Zealand. Kundi hilo lilijumuisha kampuni tano (5) zinazojishughulisha na utoaji wa mikopo na utekelezaji wa miradi ya nishati.
Wawakilishi hao wanaotoka makampuni ya NZ MFAT, CAMCO, Geoflow Imaging (GFI), JACOBS na Wyborn Capital walimweleza Balozi Luvanda nia yao ya kuwekeza kwenye miradi ya nishati ikiwemo uzalishaji wa umeme kwa kutumia jotoardhi na usambazaji wa umeme.
Kwa upande wake, Balozi Luvanda aliwaeleza wawekezaji na wafanyabiashara hao kwamba Serikali ya Tanzania iko tayari kufanya kazi na wawekezaji na ndiyo maana imeweka mazingira wezeshi ili kurahisha uwekezaji wao nchini. Alitumia fursa hiyo kuwahamasisha waje nchini kuwekeza kwenye sekta nyinginezo kama vile, utalii, kilimo, madini na uchumi wa buluu ambazo zinakuwa kwa kasi kubwa.
