Tarehe 18 Februari 2026, Balozi Anderson Mutatembwa alishiriki hafla ya kufunga Mpango wa Mafunzo ya Ufundi Viwandani ulioandaliwa na UNIDO ITPO Tokyo kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kupitia Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda (METI). Hafla hiyo ilihudhuriwa na baadhi ya Balozi za nchi za Afrika pamoja na makampuni sita ya Japan yaliyotekeleza programu hiyo. Ilielezwa kuwa mafunzo hayo (yaliyofanyika mwaka 2023 hadi 2025) yalilenga kuhamisha teknolojia za viwandani na kujenga uwezo wa rasilimali watu kupitia mfumo wa “Training of Trainers (ToT)”, ambapo washiriki zaidi ya 1,100 kutoka nchi tisa walipata mafunzo katika teknolojia nane kwa ushirikiano na taasisi tisa za mafunzo na makampuni sita ya Japan.
Mafunzo yalitekelezwa kwa mfumo wa vitendo ambapo wakufunzi walipata mafunzo nchini Japan na baadaye kuyasambaza kwa wataalamu katika nchi zao. Sekta zilizohusishwa ni pamoja na kilimo cha kisasa, usimamizi wa taka na mazingira, miundombinu ya barabara, nishati mbadala, afya ya hedhi na teknolojia ya urejelezaji wa magari chakavu (End-of-Life Vehicles – ELV), yakilenga kuongeza ujuzi wa vitendo; ajira kwa vijana na wanawake; na maendeleo ya viwanda.
Kwa upande wa Tanzania, mafunzo yalifanyika kwa ushirikiano na Kampuni ya Kaiho iliyopo Kanazawa, Japan, ambapo wakufunzi wawili kutoka VETA walipata mafunzo ya kina kuhusu ubanguaji salama wa magari, uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa vipuri. Baada ya kurejea nchini, waliendesha mafunzo kwa takribani wakufunzi na wataalamu 50, hivyo kuongeza uwezo wa ndani na kuanzisha mtandao wa wakufunzi katika sekta ya urejelezaji wa magari.
Aidha, ilisisitizwa kuwa programu hiyo ni mfano bora wa ushirikiano wa Japan, UNIDO na nchi za Afrika katika kuhamisha teknolojia na kukuza ujuzi wa viwandani. Pia, UNIDO ilieleza nia ya kuendeleza programu zinazolenga Afrika, huku ikisisitiza umuhimu wa uendelevu wa mafunzo kupitia ufuatiliaji wa matokeo, kuimarisha ToT, na ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi za mafunzo, sekta binafsi na Serikali.



