Ujumbe wa Kampuni ya JGC ya Japan, kampuni tanzu ya JGC Holdings Corporation inayoshughulika na masuala ya nishati, afya, miundombinu na mazingira, upo nchini Tanzania kwa ziara maalum kuanzia tarehe 22 hadi 25 Oktoba 2024. Lengo la ziara hiyo ni kubaini fursa za ushirikiano wa ubia na Tanzania katika masuala ya nishati hususan, kwenye miradi ya mafuta na gesi ikiwa ni pamoja na LNG.

Kampuni hiyo imefanya mazungumzo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), tarehe 22 Oktoba 2024 na inaendelea na ratiba yake ya mazungumzo na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Ujumbe huo unaoongozwa na Bw. Naoki Noguchi, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa JGC, utaendelea na mazungumzo na wizara pamoja na taasisi mbalimbali za nishati nchini hadi kuitimishwa kwa ziara hiyo, tarehe 25 Oktoba 2024.

Mnamo mwaka 2018, JGC ilishirikiana na Wizara ya Nishati katika kuandaa Mpango wa Matumizi ya Gesi Asilia nchini; na ilihamasika zaidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania kupitia Kampeni ya Kutangaza Fursa za Uwekezaji Tanzania iliyofanyika nchini Japan, tarehe 26 Mei - 8 Juni 2024 iliyoongozwa na Balozi Baraka Luvanda na Bw. Gilead Teri, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC.