Tarehe 7 Juni 2023, Ubalozi ulifanya ziara katika Chuo Kikuu cha Osaka kilichopo Osaka, Japan na kufanya mazungumzo na Prof. Tekemura Keiko, Mkuu wa Kitivo cha Lugha za Kigeni chuoni hapo. Bi. Edna Dioniz Chuku, Afisa Ubalozi aliyemwakilisha Mhe. Balozi Baraka Luvanda katika ziara hiyo iliyolenga ushirikiano katika uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili nchini Japan ambapo, Chuo Kikuu cha Osaka ni miongoni mwa vyuo vikuu vinavyofundisha Lugha ya Kiswahili.
Akiwasilisha historia fupi ya kuanza kufundishwa kwa Kozi ya Kiswahili katika chuo hicho, Prof. Keiko alieleza kuwa Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Osaka ilianzishwa mnamo mwaka 1986 wakati huo Chuo kikijulikana kama Chuo Kikuu cha Masomo ya Kigeni cha Osaka. Alieleza kuwa Kitivo cha Masomo ya Lugha za Kigeni kwa sasa chuoni hapo kina Idara 25 ambapo, Idara ya Kiswahili ni miongoni mwa idara zilizopo inayosimamia Lugha ya Kiswahili na ni idara pekee inayohusu Afrika. Alibainisha kuwa Idara zingine 24 zilizosalia zinasimamia lugha kutoka mataifa ya Asia, Ulaya na Amerika.
Prof. Keiko aliendelea kueleza kuwa somo la Kiswahili lilianza kufundishwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1980, ikiwa ni kabla ya kuanzishwa kwa idara husika mwaka 1986; na mpaka sasa wanafunzi wapatao 700 wameshanufaika na mafunzo hayo. Alieleza kuwa chuo hicho kwa sasa kinatoa Shahada ya Kwanza ya Kiswahili na ni chuo pekee nchini Japan, kinachofundisha Kiswahili kama kozi inayojitegemea; ambapo, wanafunzi husoma kwa muda wa miaka mitatu; na wastani wa wanafunzi wa Kiswahili wanaopekelewa chuoni hapo kila mwaka ni 18 hadi 20.
Baada ya kupokea historia hiyo fupi kuhusu ufundishaji wa Kiswahili chuoni hapo, Ubalozi ulimhakikishia Prof. Keiko ushirikiano wa muda wote utakaohitajika na chuo hicho katika kuwezesha ufundishaji wa lugha hiyo. Ubalozi ulitumia fursa hiyo kuwasilisha taarifa ya kuandaliwa kwa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, inayoadhimishwa duniani kote tarehe 7 Julai ya kila mwaka.
Aidha, Ubalozi uliomba ushirikiano wa chuo kikuu hicho kwa kuteua wanafunzi watakaowasilisha mada kuhusu Kiswahili ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo ya Siku ya Kiswahili Duniani. Ubalozi ulimjulisha Prof. Keiko kuwa ulikusudia kuadhimisha siku hiyo muhimu ambapo uzinduzi wake utafanyika tarehe 2 Julai 2023 na kuhitimishwa tarehe 7 Julai 2023. Ilielezwa kuwa, kama ilivyokuwa katika maadhimisho ya mwaka jana, wanafunzi wa Kiswahili katika vyuo mbalimbali vya Japan kikiwemo Chuo Kikuu cha Osaka pamoja na Wajapan walioishi Tanzania watashirikishwa katika shughuli mbalimbali za maadhimisho.
Prof. Keiko aliushukuru Ubalozi kwa kuwashirikisha katika mipango ya Maadhimisho ya Lugha ya Kiswahili na akaahidi kuteua wanafunzi watakaojumuika katika maadhimisho hayo.




