Tarehe 27 Septemba 2022, Waziri Mkuu Majaliwa alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye shughuli ya mazishi ya kitaifa ya Hayati Shinzo Abe, Waziri Mkuu Mstaafu wa Japan, akiambatana na Mama Mary Majaliwa; Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; na Balozi Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan na mkewe Bi. Consolata Luvanda. Mazishi hayo ya kitaifa yalifanyika kwenye ukumbi wa Nippon, Budokan jijini Tokyo.
Baada ya tukio la kutoa heshima za mwisho na kuweka mashada ya maua, Waziri Mkuu Majaliwa akiambatana na Mama Mary Majaliwa pamoja na Viongozi wengine kutoka nchi mbalimbali alipata fursa ya kusalimiana na kutoa pole kwa Waziri Mkuu wa Japan, Bw. Fumio Kishida na mjane wa Hayati Shinzo Abe, Bibi Akie Abe katika Kasri la kifalme la Akasaka.
Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa miongoni mwa viongozi wengine 40 wa kitaifa ambao walipata fursa hiyo. Viongozi wengine wa kitaifa walioshiriki mazishi hayo ni Marais kutoka Vietnam na Sri Lanka; Makamu wa Rais kutoka Marekani, Indonesia na Ufilipino; Marais wastaafu wa Ufaransa, Ujerumani, Mfalme wa Falme za Kiarabu, mtawala wa Qatar na Amiri wa Kuwait; pamoja na Waziri Wakuu 16 akiwemo, wa Tanzania. Wengine waliohudhuria ni Mawaziri Wakuu wastaafu, Maspika, Majaji, Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mabalozi. Nchi na mashirika zilizowasilisha salamu za rambirambi zilitambuliwa kwa kusomwa majina yao.



