Tarehe 28 Septemba 2022 alasiri, Waziri Mkuu Majaliwa alikutana na kusalimiana na Jumuiya ya Watanzania waishio Japan (Diaspora) ijulikanayo kama Tanzanite Society ambayo ina wanachama takribani 400 waliojiajiri, kuajiriwa pamoja na wanafunzi walioko katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Japan. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka Diaspora hao watambue fursa zilizopo nchini na kuzisemea vizuri ili iwe fursa ya kupata wawekezaji ambao watakuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na ikibidi wafanye ubia na wawekezaji hao. Aidha, aliwahimiza wana-Diaspora hao kutafuta marafiki wa kwenda kuwekeza nyumbani kwenye sekta mbalimbali kama vile utalii, huduma, kilimo, miundombinu, ujenzi wa majengo, madini na viwanda kwani nchi inawategemea wao kupata wawekezaji ambao ni makini kwa kuwa ndio wanaoishi nao na kuwajua zaidi.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo, uboreshaji katika sekta za elimu, afya, maji, nishati, usafiri na usafirishaji na miundombinu ya barabara na reli. Alitoa mfano wa sekta ya afya ambapo, Serikali imeweza kujenga zaidi ya vituo vya afya 670 vyenye vyumba vya upasuaji, maabara, jengo la mama na mtoto, sehemu ya kutolea dawa na chumba cha kuhifadhia maiti. Alieleza kuwa katika kila Halmashauri, Serikali imejenga hospitali na kwamba kila mkoa na kanda kuna hospital ambazo zinatoa huduma za kibingwa.
Akitoa mfano wa sekta ya maji, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa katika kuhakikisha huduma ya maji safi inawafikia wananchi, Serikali imejenga miradi mikubwa ya maji katika miji ya Bunda, Butiama, Bukoba, Tarime, Rorya ambayo yote inatumia maji ya Ziwa Victoria. Mradi mwingine wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Nzega, Tabora na Igunga wenye thamani ya shilingi ya shilingi bilioni 550 ambao unaendelea vizuri. Pia, aliuelezea mradi wa maji wa miji 28 kwa ufadhili kutoka Benki ya Exim ya India.
Kuhusu barabara, Waziri Mkuu alieleza kuwa Serikali imekamilisha barabara kuu za kuunganisha mikoa isipokuwa barabara mbili tu mkoani Kigoma na inaendelea kuunganisha wilaya kwa wilaya kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA).
Waziri Mkuu Majaliwa aliwaeleza wana-Diaspora kuwa sehemu nyingi ambazo ametembelea kumekuwa na kilio cha siku nyingi cha uraia pacha na akaeleza kuwa suala hilo ni nyeti kwa usalama wa nchi na hivyo mchakato wake unachukua muda mrefu. Aliwahakikishia kuwa azma ya kufikia hatua hiyo ipo katika hatua mbalimbali ambapo Serikali ipo katika hatua nzuri ya kutoa hadhi maalumu.
Mapema akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Japan, Bw. Frank Semaganga, alieleza kuwa jumuiya hiyo yenye wanachama 400 ilianzishwa ili waweze kusaidiana, kuleta mshikamano na kuitangaza Tanzania. Aliomba Serikali iangalie uwezekano kuboresha mifumo ya uendeshaji kwenye Soko la Hisa (DSE) ili wana-Diaspora waweze kuwekeza kwa kununua hatifungani pindi zinapotangazwa.
Aidha, Bw. Semaganga alielezea changamoto ya upatikanaji wa Kitambulisho cha Taifa kupitia Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) ikiwemo, kuchukua muda mrefu kuchakata maombi na gharama za kusafiri kwenda Tanzania kupata huduma hiyo. Hivyo, aliiomba Serikali iangalie uwezekano wa kitambulisho hicho kupatikana kupitia Ubalozi kama ilivyo kwa upande wa pasi za kusafiria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wanaosoma Japan (Tanzania Students in Japan - TSJ) Bi. Eunice Likotiko, aliiomba Serikali iangalie namna ya kutumia vizuri ujuzi wa watanzania wanaohitimu masomo yao nje ya nchi wanaporejea nchini kwa kuwa wengi wao huachwa bila kutumiwa. Aidha, aliiomba Serikali kupitia Wizara husika kuunda kanzidata ya wanafunzi waliosoma nje ya nchi na kuainisha ujuzi walioupata ili wapate fursa ya kuonesha utaalamu wao.
Bi Likotiko alipendekeza ikiwezekana Serikali itenge siku maalum ya kutambua utaalamu wa watu wanaohitimu nje ya nchi na kuipatia jina mahsusi kama vile, “Siku ya Uvumbuzi” ambapo utaalamu wao unaweza kujulikana na kuweza kutumika.
Waziri Mkuu Majaliwa alihitimisha mkutano kwa kuwasihi watumie fursa yao ya kuwepo nchini Japan kukuza lugha ya Kiswahili kama njia ya kukuza ajira kwani nchi nyingine zimeona fursa hiyo na zimeamua kukiweka Kiswahili kwenye mitaala yao (syllabus). Aliwaeleza kuwa wanaweza kufanya hivyo kwa kushirikiana na Ofisi za Ubalozi kuanzisha madarasa ya Kiswahili pamoja na kuandaa majarida na machapisho kwa lugha ya Kiswahili kama njia mojawapo ya kuibidhaisha lugha hiyo.

