Ubalozi uliratibu na kufanikisha kukamilika kwa uwekaji saini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Tumbaku ya Japan (Japan Tobacco – JT), uliofanyika tarehe 12 Septemba 2023, jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. MoU hiyo ilisainiwa na Mhe. Dkt. Festo John Dugange, Naibu Waziri wa Ofisi ya Nchi – TAMISEMI kwa niaba ya Serikali; na Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Bw. Masamichi Terabatake kwa upande wa JT.
Lengo kuu la kuwa na Makubaliano hayo (MoU) ni kurasimisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii (afya, maji na elimu) iliyopo katika maeneo yanayolima tumbaku nchini, ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kijamii (Corporate Social Responsibility – CSR) inayotekelezwa na kampuni hiyo. Hivyo, kupitia Makubaliano hayo, JT imedhamiria kutumia kiasi cha dola za Marekani 1,260,000 kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025 sawa na dola za Marekani 420,000 kwa mwaka kwa ajili ya kufadhili miradi hiyo. Aidha, kwa mwaka 2022 kampuni hiyo ilitumia dola za Marekani 593,000 kutekeleza miradi mbalimbali nchini ikiwemo, ujenzi wa shule, mabweni, na miradi ya maji katika mikoa ya Tabora na Singida.
Kampuni ya Japan Tobacco (JT) ambayo zamani ilijulikana kama Japan Tobacco Inc (JTI) ni kampuni ya kimataifa inayojishughulisha na biashara ya tumbaku duniani. Nchini Tanzania, JT inajishughulisha na ununuzi wa tumbaku katika mikoa inayolima tumbaku nchini na pia imewekeza kwa umiliki wa asilimia 75 katika Kiwanda cha Utengenezaji Sigara cha Tanzania Cigaratte Company (TCC Plc.) kilichoanzishwa mwaka 1961. JT kupitia ununuzi wa tumbaku nchini na uwekezaji wao katika kiwanda cha sigara cha TCC Plc., imeajiri wafanyakazi zaidi ya 440 na kuwa na matawi 16 nchini Tanzania.
Aidha, walipokutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwezi Septemba 2022 jijini Tokyo, JT waliahidi kuwa watakuwa na uwezo wa kununua tani 30,000 za tumbaku kutoka Tanzania kwa mwaka. Kiasi hicho ni mara mbili zaidi ya kiasi cha tumbaku inayozalishwa nchini. Hivyo, hii ni fursa kwa watanzania kuzalisha zaidi zao hilo kwa kuwa soko la uhakika lipo.




