Bi. Midori Uno ameandaa Makala ya kuielezea Lugha ya Kiswahili na namna ilivyoadhimishwa Duniani na kwa upekee wake nchini Japan. Bi. Uno alikuwa Mdhamini wa Shindano la Kuwasilisha Mada kwa Lugha ya Kiswahili na pia miongoni mwa Majaji wa Shindano hilo, lililofanyika kama moja ya tukio muhimu la kusheherekea Siku ya Maadhimisho ya Kiswahili Duniani. Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan tarehe 9 Julai 2022, kwenye Ofisi za Ubalozi, Tokyo. Makala ya Bi. Uno imechapishwa kwenye Gazeti la Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) linalotoka kila mwezi.
Nukuu ya Makala husika:
SIKU YA KISWAHILI DUNIANI
Mwaka jana UNESCO ilitangaza kwamba tarehe saba mwezi wa saba kuwa Siku ya Kiswahili Duniani. Siku hii ya tarehe saba mwezi wa saba ndiyo siku maalum kwa Tanzania yaani siku ya kuundwa kwa Chama cha TANU kilichopigania uhuru wa Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, na Kiswahili kilichaguliwa kuwa lugha ya kitaifa, kikaunganisha makabila zaidi ya 260. Kwa hiyo Tanzania imepata kuwa nchi ya amani tele Barani Afrika.
Ubalozi wa Tanzania nchini Japani uliadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani kwa kupanga mashindano ya kutoa hotuba kwa lugha hii tukufu ya Kiswahili ukitangaza hadharani kuwaalika watoaji hotuba.
Mashindano hayo yalifanyika hapo tarehe tisa mwezi wa saba Jumamosi na niliona fahari kwa kuteuliwa kuwa mmojawapo wa majaji watatu wa siku hiyo.
Ninausifu sana uamuzi wa Mheshimiwa Balozi Luvanda wa Tanzania na watumishi wa Ubalozi kupanga mashindano hayo chini ya ugonjwa wa COVID 19 kuwepo humu nchini na tena ninazisifu jitihada zao kubwa za utendaji safi na uongozi mzuri kwa tukio hili maalum.
Ili kuwakusanya watoaji hotuba wengi, nilijitahidi kuwashaushi wale waliokuwa vijana wa kujitolea wa JICA na wanafunzi wangu nilipowafundisha Kiswahili katika vyuo vikuu na shule nyingine. Nilifurahi sana kujua kwamba watu 21 walijiandikisha. Na kwanza upande wa Ubalozi uliwachagua 11 kati yao, na nilifurahi kuyaona majina matatu ya wale waliokuwa vijana wa kujitolea nchini Tanzania, Bw. Mikado Araki, Bi. Masami Sumi na Bi. Tokoro Miho.
Siku ya mashindano, hapo tarehe tisa mwezi wa saba, shughuli zilianzishwa saa tatu na nusu asubuhi, na matokeo yake yailtangazwa baada ya kula chakula cha mchana. Kwa hisani ya Ubalozi tuliweza kuonja vyakula vitamu mbalimbali vya Kitanzania bila kukosa Ugali kwa hiyo tulishukuru sana Ubalozi kwa maandalizi yake mazuri.
Kuwachagua washindi kulikuwa kazi ngumu, kwani kila mtoaji alitoa hotuba nzuri sana, kwa hiyo hatukuwa na budi kuwachagua chini ya misingi ya Kufikisha dhumuni, Kuonyesha hisia, Maswali na majibu. Kama matokeo, nafasi ya kwanza ilipewa Bi Masami Sumi aliyekuwa kijana wa kujitolea nchini Tanzania mwaka 2017, na huyu ndiye mwanafunzi wangu wakati wa kufundisha Kiswahili katika kimojawapo cha vyuo vikuu, na tena nafasi ya tatu pia alikuwa mwanafunzi wangu katika Chuo Kikuu, Bi Yasuko Togashi.
Mimi mwenyewe pia nilikuwa kijana wa kujitolea wa kwanza nchini Tanzania. Na wakati huo nilijitahidi sana kujifunza Kiswahili katika kozi ya jioni ya Chuo Kikuu cha DSM. Na baada ya kurejea humu nchini nliiunga mkono na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Japani. Na pia nilifundisha Kiswaili katika chuo cha mafunzo cha Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Japani na vyuo vikuu. Na wakati huo huo nilitunga vitabu vingi kama vile kitabu cha sarufi cha Kiswahili, kamusi mbili za Kiswahili-Kijapani na Kijapani-Kiswahili, kitabu cha picha za Tingatinga na vitabu vingine kuhusu Tanzania na kadhalika. BAKITA ilinipatia hati ya shukurani kwa ajili ya jitihada zangu za kueneza Kiswahili nchini Japani.
Kwa hiyo kwangu mimi, siku ya mashindano hayo ya Kiswahili na pia siku ya Kiswahili Duniani zimepata kuwa kumbukumbu nzuri na za furaha tele zisizosahaulika milele.
IMEANDIKWA NA BI. MIDORI UNO
NA KUCHAPISHWA KWENYE GAZETI LA MAENDELEO LA JAPAN (JICA)