Tarehe 3 hadi 4 Juni 2023, Timu ya Tanzania ya Softball kwa Wanawake chini ya miaka 15 ilishiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Kuwania Kombe la Utsugi (Utsugi Cup) yaliyofanyika mjini Takasaki, Gunma, Japan. Ujumbe wa timu hiyo ulijumuisha wachezaji 16, walioambatana na walimu watatu (03) wa Shule za Sekondari za Tanzania, kocha wa timu, mwakilishi kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Baseball Tanzania (TaBSA), wakiongozwa na Rais wa Japan-Africa Baseball & Softball Foundation (J-ABS), Bw. SHINYA Tomonari ambaye pia ni Kocha Mkuu wa timu hiyo. Ubalozi uliwakilishwa na Bi. Edna Dioniz Chuku na Bw. Hosea Chikolongo waliojumuika pamoja na Ujumbe wa Tanzania.
Mashindano ya Utsugi Cup yaliyoandaliwa na Bi. Taeko Utsugi ambaye ndiye Muasisi wa mashindano hayo yalishirikisha timu sita kutoka Tanzania, Japan, Marekani, China, Italia na Mexico. Kufanyika kwa mashindano hayo ni maandalizi ya Mashindano ya kuwania Kombe la Dunia la Softball la Wanawake chini ya miaka 15 (U-15 Women’s Softball World Cup) yanayotarajiwa kufanyika nchini Japan, mwezi Oktoba 2023.
Kupitia mashindano hayo ambapo, Tanzania ilishika nafasi ya sita kumechangia kwa kiasi kikubwa kudumishwa kwa Diplomasia ya Michezo baina ya Tanzania na nchi zilizoshiriki. Aidha, Tanzania ilipewa heshima ya kuwa mshiriki pekee kutoka Bara la Afrika ikiwa ni katika kutambua kuwa Tanzania ni chimbuko la mchezo wa baseball na softball kwa upande wa Afrika.






