Tarehe 22 Juni 2024, Ubalozi ulishiriki kwenye Hafla ya Mahafali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Japan (International University of Japan - IUJ) kilichopo Niigata, Japan. Katika Mahafali hayo, Watanzania watatu (03) walitunukiwa Shahada ya Umahiri (Masters degree), katika fani za uchumi na biashara. Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda ambaye ni mlezi wa wanafunzi watanzania wanaosoma Japan, aliwakilishwa katika Mahafali hayo na Afisa Ubalozi - Bi. Edna Dioniz Chuku.
Ikiwa ni sehemu ya Mahafali hayo, wanafunzi bora tisa (9) walitunukiwa cheti cha heshima cha utambuzi katika masuala ya biashara cha Beta Gamma Sigma (BGS) - the International Business Honor Society ambapo, Mtanzania, Bi. Glory Henry, ni miongoni mwa wahitimu aliyetunukuwa cheti hicho.
Aidha, kabla ya kuanza kwa hafla hiyo, Ubalozi ulipata wasaa wa kuwa na mazungumzo na viongozi wa Chuo wakiwemo, Mwenyekiti na Makamu Mkuu wa Chuo. Majadiliano yalijikita katika namna ya kuendeleza ushirikiano kati ya IUJ na Tanzania.
Watanzania ni miongoni mwa wanufaika wa fursa za elimu na ufadhili wa masomo nchini Japan, zinazotolewa na Serikali ya Japan, mashirika, taasisi au vyuo vikuu vya nchini humo.