Tarehe 18 Machi 2026, Balozi Anderson Mutatembwa alifanya mazungumzo na Bw. Susumu Tsubaki, Afisa Mtendaji Mkuu wa AAIC Holdings Pte. Ltd., kuhusu maendeleo ya uwekezaji wa kampuni yao (TANJA) iliyowekeza nchini katika sekta ya kilimo cha kibiashara. Ilielezwa kuwa kampuni hiyo imewekeza katika shamba la kahawa aina ya Arabica lenye takribani hekta 1,700 katika eneo la Karatu, na kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 250 kwa mwaka, ambapo zaidi ya asilimia 80 husafirishwa kwenda Japan chini ya chapa ya “Ngorongoro Coffee.”
Taarifa ilitolewa kuwa uwekezaji huo umechangia ajira kwa wananchi (wafanyakazi wa kudumu 350 na wa msimu zaidi ya 300) pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii kupitia Smart Village Initiative, ikijumuisha maji safi, nishati jadidifu, elimu, afya na huduma za kidijitali. Aidha, kampuni hiyo inaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wanawake, kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kusaidia sekta ya elimu kupitia lishe mashuleni na miradi ya kilimo shuleni.
Kuhusu mipango ya baadaye, kampuni hiyo inapanga kuongeza wigo wa uwekezaji katika mazao mengine ikiwemo parachichi, macadamia na chai ya kijani. Kwa sasa ina zaidi ya hekta 100 za parachichi na inalenga kufikia hekta 2,000, huku ikisisitiza umuhimu wa Tanzania kuharakisha ufunguzi wa soko la parachichi ya Tanzania nchini Japan kupitia kukamilisha taratibu za udhibiti na ithibati (phytosanitary approvals), kwa lengo la kuanza mauzo ya moja kwa moja ifikapo mwaka 2029.
Aidha, Bw. Tsubaki alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya Hati ya Ushirikiano (MOU) ya Utatu baina ya TANJA, Kampuni ya Key Coffee ya Japan na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), yenye lengo la kuwawezesha wakulima wadogo wa kahawa katika mikoa ya Kaskazini. Alibainisha kuwa rasimu ya MOU tayari imewasilishwa na ipo katika hatua za mapitio kwa upande wa Tanzania, na matarajio yao kuwa itasainiwa hivi karibuni ili kuwezesha utekelezaji wa programu za kuongeza tija, ubora na upatikanaji wa masoko ya kahawa ya wakulima wadogo.
Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa alishukuru uwekezaji huo unaoendelea kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii nchini, na kupongeza juhudi za kampuni katika kuongeza thamani ya mazao na kukuza ajira. Aidha, alimhakikishia Bw. Tsubaki kuharakishwa kwa hatua za kukamilisha MOU ya Utatu; na pia kufuatilia kwa ukaribu kwa mamlaka husika za Tanzania na Japan ili kufanikisha ufunguzi wa soko la parachichi. Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika uhamishaji wa teknolojia, ujuzi na uwekezaji endelevu katika sekta ya kilimo.



