Tarehe 24 Machi 2026, Balozi Anderson Mutatembwa alitembelea Makao Makuu ya Shirika la Taifa la Utangazaji la Japan (NHK World) jijini Tokyo, ambapo alifanya mazungumzo na Makamu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo. Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano katika sekta ya habari kati ya Tanzania na Japan, pamoja na kuangazia fursa zilizopo katika kukuza uelewa wa kimataifa kuhusu Tanzania kupitia vyombo vya habari vya Japan.

Baada ya mazungumzo hayo, Mheshimiwa Balozi alipata wasaa wa kutembezwa katika ofisi za Shirika hilo na kujionea shughuli mbalimbali za uendeshaji na uzalishaji wa vipindi. Aidha, alipata fursa ya kufanya mahojiano maalum, ambapo alizungumzia uhusiano wa Tanzania na Japan, fursa za uwekezaji na biashara, uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili nchini Japan, pamoja na manufaa ya kuendeleza ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.