Tarehe 19 Machi 2026, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa, alifanya mazungumzo na Rais wa Chuo Kikuu cha Tokyo cha Masomo ya Kigeni (University of Foreign Studies -TUFS), Profesa Nobou Haruna, yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kitamaduni kati ya Tanzania na Japan. Katika mazungumzo hayo, Profesa Haruna alieleza kuwa Chuo hicho ni moja ya vyuo vikuu vinavyojikita katika masomo ya lugha za kigeni na tafiti za kimataifa na kinatoa mafunzo ya takribani lugha 80 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Aidha, alibainisha kuwa programu ya masomo ya lugha ya Kiswahili katika Chuo hicho ilianza rasmi mwaka 2019 na imekuwa ikipata mwitikio mkubwa kutoka kwa wanafunzi wa Japan. Alieleza kuwa idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 17 mwaka 2019 hadi kufikia takribani wanafunzi 75 mwaka 2025, hali inayoonesha kuongezeka kwa hamasa ya wanafunzi wa Japan kujifunza lugha ya Kiswahili pamoja na kuifahamu Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki. Hata hivyo, Profesa Haruna alieleza kuwa kwa sasa Chuo hicho hakina ushirikiano rasmi wa kitaaluma na vyuo vikuu vya Tanzania licha ya kuwepo kwa mawasiliano na ushirikiano katika baadhi ya tafiti na shughuli za kitaaluma.
Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa alikishukuru Chuo hicho kwa kuanzisha mafunzo ya lugha ya Kiswahili ambayo yamechangia kukuza uelewa wa lugha na utamaduni wa Tanzania nchini Japan. Aidha, alimpongeza Profesa Daisuke Shinagawa wa TUFS kwa mchango wake katika kuandaa Kamusi ya Kijapani–Kiswahili kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es salaam hatua inayosaidia kuimarisha mawasiliano na tafiti za lugha kati ya nchi hizo mbili.
Vilevile, Balozi Mutatembwa alikishukuru Chuo hicho kwa kutoa fursa kwa Mabalozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ikiwemo Tanzania, kutoa mihadhara kwa wanafunzi wa Chuo hicho kuhusu nchi zao kupitia mpango wa SADC Lecture Series, ambao umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na nchi nyingine za SADC katika jamii ya kitaaluma nchini Japan.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Mutatembwa alipendekeza kuanzishwa kwa ushirikiano rasmi wa kitaaluma na vyuo vikuu vya Tanzania hususan Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Alieleza kuwa ushirikiano huo unaweza kujumuisha kubadilishana wakufunzi na wanafunzi, hususan katika masomo ya lugha ya Kijapani na Kiswahili,utamaduni pamoja na kufanya tafiti za pamoja katika masuala ya lugha, utamaduni na tafiti za Afrika.



