Tarehe 16 Oktoba 2022, Ubalozi uliratibu ushiriki wa timu ya riadha ya Tanzania katika Mashindano ya “Nagai Marathon 2022” yaliyofanyika katika jiji la Nagai. Ujumbe wa timu hiyo ilijumuisha wanariadha wanne wakiwemo, Alphonce Simbu, Fabiano Joseph, Anjelina Yumba na Jafary Ngimba, ukiongozwa na mwanariadha mstaafu, Bw. Juma Ikangaa na Kocha wa timu, Bw. Francis Marcially.

Mashindano hayo ya “Nagai Marathon 2022” yaliyoandaliwa na Jiji la Nagai yalishirikisha wanariadha wapatao 800 kutoka Japan na Tanzania kwa lengo la kukuza ushirikiano katika sekta ya michezo. Watanzania Alphonce Simbu na Fabiano Joseph waliibuka kidedea kwa ushindi wa nafasi ya kwanza kwa mbio za kilometa 21 na kilometa 42, mtawalia. 

Tanzania na Mji wa Nagai zimekuwa na ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu tangu mwaka 2015 ukiwa na manufaa kwa pande zote mbili kupitia nyanja za kijamii, sanaa, michezo na utamaduni. Mathalan, mwaka 2019 Mji wa Nagai uliialika timu ya riadha ya Tanzania kushiriki kwenye mashindano ya “Nagai Marathon 2019”; na pia mwaka 2021 mji huo ulikuwa mwenyeji wa Timu ya Taifa ya Olimpiki ya Tanzania iliyoshiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020. 

Hata baada ya kuhitimishwa kwa Mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020, Mji wa Nagai umeendeleza mawasiliano ya karibu na Tanzania na kurasimisha ushirikiano kati ya mji huo wa Nagai na Baraza la Michezo Tanzania; na hivyo kuwezesha fursa za mafunzo ya michezo kwa wataalamu wa Tanzania mjini Nagai. Aidha, mji wa Nagai umedhamiria kuwa na ushirikiano wa kidugu kati yake na jiji la Dodoma na hivyo kufungua fursa nyingi za ushirikiano zitakazonufaisha pande husika.