Ubalozi unapenda kutoa taarifa kuhusu uwepo wa fursa mbalimbali za ufadhili wa masomo na tafiti nchini Japan, zinazotolewa na Serikali ya Japan na wadau wengine wa maendeleo waliopo Japan, kama ifuatavyo:
i) Serikali ya Japan kupitia Wizara ya Elimu, Utamaduni, Michezo, Sayansi na Teknolojia (MEXT Scholarship);
ii) Programu za Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) – programu za JICA hutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa watumishi wa umma, wataalamu, wanasayansi na viongozi wa taasisi mbalimbali kutoka Tanzania;
iii) Mashirika binafsi ya Kijapani yanayotoa ufadhili wa kujitegemea kwa wanafunzi wa kimataifa; na
iv) Vyuo vikuu vinavyotoa ufadhili moja kwa moja (University-Specific Scholarships) kwa wanafunzi wa kimataifa.
Sehemu kubwa ya ufadhili huu unalenga masomo kwa ngazi ya Umahiri (Master’s) na Uzamivu (PhD). Aidha, Wizara ya Elimu ya Japan hutoa ufadhili kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza (Undergraduate) na Masomo ya Ufundi (Specialized Training).
Kwa taarifa zaidi kuhusu fursa hizo, zikiwemo sifa za waombaji na taratibu za maombi, tafadhali tembelea tovuti:
UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN: https://www.jp.tzembassy.go.tz/resources/view/taarifa-ya-fursa-mbalimbali-za-ufadhili-wa-masomo-na-tafiti-zilizopo-nchini-japan-scholarships-for-international-students-in-japan
UBALOZI WA JAPAN NCHINI TANZANIA: https://www.tz.emb-japan.go.jp/itprtop_en/index.html
STUDY IN JAPAN – Scholarship Pamphlet: https://www.studyinjapan.go.jp/en/planning/brochures/#002
Tunashauri Watanzania wenye nia ya kusoma au kufanya tafiti nchini Japan kutembelea tovuti hizi mara kwa mara ili kubaini fursa mpya zinapowekwa kwa mwaka husika wa masomo. Ubalozi unatoa rai kwa Watanzania wote wenye nia, sifa na vigezo vinavyohitajika, kuchangamkia fursa hizo, zinapotangazwa.
UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN
TOKYO
11 NOVEMBA 2025
