Leo, tarehe 11 Novemba 2025, Ubalozi umepokea wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha SOKA kilichopo Tokyo, Japan. Lengo la ziara hiyo lilikuwa kutoa taarifa kuhusu maandalizi yanayoendela ya Shindano la 35 la Hotuba kwa Lugha ya Kiswahili, litakalofanyika tarehe 30 Novemba 2025, katika chuo hicho.

Chuo Kikuu cha SOKA kimekuwa kikiandaa Mashindano ya Hotuba kwa Lugha ya Kiswahili kila mwaka tangu kuasisiwa kwa mashindano hayo mnamo mwaka 1991 na Mwasisi wa Chuo hicho, Dkt. Daisaku Ikeda. Mashindano haya yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza uelewa wa Lugha ya Kiswahili na utamaduni wake miongoni mwa Wajapani, sambamba na kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni kati ya Tanzania na Japan.

Kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu ni “Wewe na Afrika”, ikilenga kuibua mitazamo ya Wajapani kuhusu bara la Afrika na kuhamasisha urafiki, mawasiliano, na uelewa wa Bara la Afrika hususan, kupitia Lugha ya Kiswahili.

Ubalozi umetumia fursa hiyo kupongeza juhudi za Chuo Kikuu cha SOKA katika kuendeleza Lugha ya Kiswahili na kukuza uhusiano wa kirafiki kati ya Tanzania na Japan kupitia elimu na utamaduni. Aidha, umeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wanafunzi hao na Chuo Kikuu cha SOKA kwa ujumla, katika juhudi hizo za kueneza Lugha ya Kiswahili nchini Japan.