Tarehe 11 Mei 2023, Ubalozi ulishiriki kwa njia ya mtandao kwenye Semina ya Kwanza (01) ya Wawekezaji na Wafanyabiashara wa Tanzania na Japan iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwenye Ofisi za Kituo cha Uwekezaji, Tanzania ambayo iliandaliwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya Ubalozi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Ubalozi wa Japan nchini Tanzania.
Semina hiyo ilihudhuriwa na washiriki wapatao 70 walioshiriki kwa njia ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao; na ilishirikisha taasisi za Serikali ya Tanzania zikiwemo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Idara ya Uhamiaji Tanzania. Washiriki wengine ni Ubalozi wa Japan nchini Tanzania, JICA, Umoja wa Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Japan waliopo Tanzania (Committee on Commerce and Industry of the Japanese Society of Tanzania - CCIJT) pamoja na wawakilishi wa wafanyabiashara wa Tanzania.
Lengo kuu ya Semina hiyo lilikuwa kujadiliana kuhusu kuweka mazingira mazuri ya kibiashara na kiuwekezaji nchini kwa kampuni za Kijapani ambapo, changamoto wanazokumbana nazo na mapendekezo ya kuzitatua vilijadiliwa kwa kina kwenye semina hiyo. Aidha, semina hiyo ilipokea mawasilisho ya kampuni mbalimbali za Japan zilizopo Tanzania, mikakati ya Serikali ya Tanzania katika kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji wa kigeni na wasilisho kutoka JICA ambapo, walielezea shughuli wanazozifanya nchini hususan, katika kukuza sekta za biashara, viwanda na uwekezaji.
Kuandaliwa kwa semina hii, kumefungua milango ya kuwa na semina za namna hii kila mwaka ambapo, semina ya pili inatazamiwa kufanyika mnamo mwezi Februari au Machi 2024 kwa lengo la kuendelea kuimarisha mazingira mazuri ya kibiashara na uwekezaji nchini hususan, kampuni na wafanyabiashara kutoka Japan.

