Leo, tarehe 20 Oktoba 2023, Ubalozi umetoa semina maalum kuhusu Tanzania kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha WASEDA kilichopo Tokyo, Japan. Semina hiyo iliyofanyika chuoni hapo ilitolewa kwa wanafunzi wapatao 70 pamoja na wahadhiri wawawili (2) wa chuo hicho ambapo, walipata fursa ya kujifunza mengi kuhusu Tanzania kupitia wasilisho la historia ya Tanzania, fursa za uwekezaji na biashara, vivutio vya utalii, utamaduni mila na desturi za Tanzania ikiwa ni pamoja na zoezi la kujifunza uvaazaji wa mavazi ya tamaduni za Tanzania.

Semina hiyo ilihitimishwa kwa fursa ya maswali na majibu ambayo yalijikita zaidi katika kuelewa historia ya Muungano wa Tanzania, uongozi na demokrasia nchini, ushirikiano wa Tanzania na mataifa mengine, namna utamaduni na matumizi ya Lugha ya Kiswahili yalivyochangia kuleta umoja ndani ya jamii ya Tanzania, vivutio na fursa za utalii, pamoja na mchango wa wanawake katika masuala ya kiuchumi  na kijamii ikiwemo, kwenye elimu, kilimo na afya.

Semina za aina hii zimekuwa zikiandaliwa na Ubalozi kila mwaka kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Japan zikiwemo, Asasi za Kiraia, shule na vyuo vikuu vya Japan kwa lengo la kujenga taswira nzuri ya nchi pamoja na kuhamasisha utalii, biashara na uwekezaji kwa umma wa Japan.