Tarehe 21 Juni 2023, Ubalozi ulitoa semina maalum kuhusu Tanzania kwa wanafunzi wa mwaka wa pili wanaosoma Masomo ya Kigeni katika Chuo Kikuu cha SOKA. Semina hiyo iliyofanyika chuoni hapo ilitolewa na Bi. Edna Dioniz Chuku, Afisa Ubalozi, kwa wanafunzi wapatao 25 pamoja na wahadhiri wanne (4) wa chuo hicho. Washiriki hao walipata fursa ya kujifunza mengi kuhusu Tanzania kupitia wasilisho la historia ya Tanzania, fursa za uwekezaji na biashara, vivutio vya utalii, utamaduni mila na desturi za Tanzania ikiwa ni pamoja na zoezi la kujifunza uvaazaji wa mavazi ya tamaduni za Tanzania.
Semina hiyo ilihitimishwa kwa fursa ya maswali na majibu ambayo yalijikita zaidi katika kuelewa historia ya Muungano wa Tanzania, uongozi na demokrasia nchini, namna utamaduni na matumizi ya Lugha ya Kiswahili yalivyochangia kuleta umoja ndani ya jamii ya Tanzania, vivutio na fursa za utalii, pamoja na mchango wa wanawake katika masuala ya kiuchumi na kijamii ikiwemo, kwenye elimu, kilimo na afya.
Chuo Kikuu cha Soka ni miongoni mwa vyuo vikuu nchini Japan vinavyofundisha Masomo ya Kigeni ikiwemo, ufundishaji wa Lugha ya Kiswahili. Chuo Kikuu hicho pia huandaa Mashindano ya Mwaka ya Hotuba kwa Lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi na raia wengine wa Japan wenye uelewa na lugha hiyo. Mashindano hayo hufanyika kila mwaka tangu kuasisiwa kwake miaka ya 1990 na Muasisi wa chuo kikuu hicho, Dkt. Daisaku Ikeda.
Aidha, Chuo Kikuu cha SOKA kimekuwa kikiandaa semina mbalimbali kwa wanafunzi wake kwa kushirikiana na balozi zenye uwakilishi nchini Japan kwa lengo la kuwajengea uelewa wanafunzi hao kuhusu tamaduni, mila na desturi za mataifa ya kigeni. Ubalozi umekuwa ukitumia fursa za uwepo wa programu mbalimbali chuoni hapo na vyuo vingine vya Japan, shule za msingi na sekondari, pamoja na taasisi zingine zikiwemo, Asasi za Kiraia kutoa semina kuhusu Tanzania kwa lengo la kujenga taswira nzuri ya nchi na kuhamasisha utalii, fursa za biashara na uwekezaji kwa umma wa Japan.


