Tarehe 26 Februari 2023, mwanariadha kutoka Tanzania, Bw. Alphonce Felix Simbu alishiriki kwenye Mashindano ya Osaka Marathon 2023 yaliyofanyika jijini Osaka, Japan. Mashindano hayo yaliandaliwa na Jiji la Osaka na kushirikisha wanariadha wapatao 32,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kukuza ushirikiano kwenye michezo. 

Bw. Simbu kutoka Tanzania aliibuka mshindi wa tatu (3) kwenye mashindano hayo katika mbio za kilometa 42 kwa kukimbia kwa muda wa masaa 2:06:19; na kuzawadiwa Medali ya Shaba miongoni mwa zawadi zingine zilizotolewa kwa washindi wa mashindano hayo. Alipowasili nchini Japan, Bw. Simbu alipokelewa na Naibu Meya wa Jiji la Nagai, Bw. Saito Tamaki, aliyeambatana na watumishi wengine wa Ofisi ya Meya ambapo, baadaye walihudhuria mashindano hayo. 

Tanzania na Mji wa Nagai zimekuwa na ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu tangu mwaka 2015 ukiwa na manufaa kwa pande zote mbili kupitia nyanja za kijamii, sanaa, michezo na utamaduni. Mwaka 2021 mji huo ulikuwa mwenyeji wa Timu ya Taifa ya Olimpiki ya Tanzania iliyoshiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020. Hata baada ya kuhitimishwa kwa Mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020, Mji wa Nagai umeendeleza mawasiliano ya karibu na Tanzania na kurasimisha ushirikiano kati ya mji huo wa Nagai na Baraza la Michezo Tanzania kupitia Makubaliano ya Ushirikiano (MoU). 

Ushirikiano huu umewezesha kupatikana kwa fursa mbalimbali kama vile, mafunzo ya michezo kwa wataalam wa Tanzania mjini Nagai. Aidha, mji wa Nagai umedhamiria kuwa na ushirikiano wa kidugu (sister cities friendship) kati yake na jiji la Dodoma na hivyo kufungua fursa nyingi za ushirikiano zitakazonufaisha pande husika.