Tarehe 30/12/2023 Balozi wa Tanzania nchini Japan Mheshimiwa Baraka Luvanda alihudhuria mkutano wa mwaka “Annual General Meeting” 2023 wa Chama cha wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini Japan “The Association of Tanzania Students in Japan - TSJ” uliofanyika katika mji wa Osaka. Katika mkutano huo masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo Chama hicho kuendelea kushirikiana na ubalozi katika kutafuta na kuzitangaza fursa zaidi za masoma kwa watanzania na namna ya kuimarisha umoja wa wanafunzi hao. Mheshimiwa Balozi aliwapongeza viongozi waliomaliza muda wao kwa kazi nzuri waliyofanya wakiwa madarakani na kuwataka viongozi wapya kuendeleza kazi hiyo kwa kipindi chote watakacho kiongoza chama hicho. Aidha mkutano huo ulitanguliwa na uchaguzi wa Viongozi wapya uliofanyika tarehe 29/12/2023 ambapo Bw.Zavuga Rumisha Zuberi kutoka Chuo cha Kumamoto alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Bw. James Reuben Yuni kutoka Chuo cha Yoshisha Makamu Mwenyekiti, Bw.Emmanuel Maduhu kutoka Chuo cha Nagasaki - Katibu, Bw.Almachius Tryphone Mutasingwa kutoka Chuo cha Kyushu - Katibu Msaidizi na Bw. Changoma Francis Marko kutoka Chuo cha Hakkaido - Mweka Hazina.