Tarehe 31 Agosti 2023, Ubalozi ulitembelewa na Ujumbe kutoka Kampuni ya ITOCHU ya Japan, miongoni mwa kampuni kubwa zinazojishughulisha na biashara ya vyakula na vinywaji nchini Japan. Ujumbe huo uliongozwa na Bw. Yuma Kanemoto, Meneja wa Mauzo, Kanda ya Afrika mwenye ofisi zake Nairobi, Kenya; ambaye aliambatana na Bw. Kanji Yamaguchi, Mratibu Mkuu wa Masuala ya Tafiti wa kampuni hiyo.
Ujumbe huo ulieleza kuwa shabaha ya ujio wao ni kuwa na maongezi na Ubalozi kuhusu taratibu za kuanza kuleta asali ya Tanzania nchini Japan. Walieleza kuwa kwa sasa Kampuni ya ITOCHU inaleta bidhaa za nafaka, kahawa na ufuta wa Tanzania hivyo, mpango wao ni kuongeza wigo wa kuanza kuleta asali ya Tanzania, kuanzia mwaka 2024.
Aidha, walibainisha kuwa ili kutimiza azma na mpango huo, tayari wameshaanza mazungumzo na baadhi ya kampuni za Tanzania zinazojishughulisha na asali. Vilevile, walieleza kuwa wamefanya utafiti kuhusu soko la asali nchini Japan na kushauri ubora na viwango vya asali kulingana na soko la Japan kwa wazalishaji wa Tanzania. Walieleza kuwa kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na Kampuni ya Swahili Honey ambapo, elimu kuhusu uvunaji wa asali ili kukidhi viwango vya Japan inaendelea kutolewa kwa wazalishaji hao.
Pia, ujumbe huo ulieleza kuwa matumaini yao ni kuwa mnamo mwaka 2024, asali ya Tanzania itaanza kuuzwa Japan kupitia ubia uliopo kati ya ITOCHU na moja ya migahawa maarufu nchini Japan ya Tully’s ambayo, kwa sasa inauza kahawa ya Tanzania. Hivyo, waliomba ushirikiano wa ubalozi katika kuitangaza asali hiyo, itakapoanza kuuzwa nchini Japan.
Ubalozi uliwashukuru ITOCHU kwa kuwa mshirika mkubwa wa biashara kwa bidhaa za Tanzania nchini Japan na jitihada za kuanzisha soko jipya la asali ya Tanzania. Ubalozi uliwahakikishia ushirikiano kama walivyoomba katika kutangaza asali ya Tanzania; pamoja na kuahidi kuwaunganisha na wazalishaji wengine wa zao hilo nchini ili kuwa na wigo mpana wa soko la asali ya Tanzania nchini Japan.


