Leo tarehe 27 Agosti 2022, Mkutano wa 8 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 8 Summit) umeanza kufanyika mjini Tunis, Tunisia. Hii ni mara ya pili kwa mkutano huu kufanyika katika ardhi ya Bara la Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 baada ya ule uliofanyika Kenya mwaka 2016 (TICAD 6).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anawakilishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa katika Mkutano huu. Mheshimiwa Kassim Majaliwa atakuwa na mazungumzo ya pembezoni na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Fumio Kishida; pamoja na baadhi ya watendaji wakuu wa kampuni na taasisi za Japan.
Mkutano wa TICAD 8 unafanyika kwa siku mbili tarehe 27 na 28 Agosti 2022; na umetanguliwa na Kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika nchini Japan, kilichofanyika tarehe 25 Agosti 2022. Pamoja na masuala mengine, Mkutano huu unatarajiwa kukubaliana kuhusu namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063).
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika.
Agenda za Mkutano wa TICAD 8 zinalenga kukabiliana na changamoto zinazoikabili Afrika zimejielekeza katika nguzo tatu muhimu ambazo ni: kulitambua Bara la Afrika kama eneo linalokua kwa kasi kiuchumi huku likikabiliana na changamoto za masuala ya kijamii; kuendelea kuifanya Afrika kuwa jamii stahimilivu na endelevu; na kuendelea kuimarisha hali ya utulivu na amani, Barani Afrika.
Agenda 2063 ilikubaliwa na viongozi wa Afrika wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika kwa lengo la kuliunganisha Bara la Afrika katika masuala ya kukuza uchumi; kuhamasisha utawala bora na utawala wa sheria; kuhakikisha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja; kuhakikisha amani na usalama unaimarika na kuiweka Afrika katika nafasi ya mchangiaji mkuu wa uchumi duniani.
Tangu kuanza kwa mikutano ya TICAD, Japan imekuwa ikiongeza kiasi cha fedha za mkopo wa masharti nafuu na msaada katika kuchangia maendeleo ya Afrika kutoka Dola za Marekani bilioni 0.6 kwa mwaka 1993 (TICAD 1) hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 20 kwa mwaka 2019 (TICAD 7). Kwa upande wa Tanzania misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka Japan imesaidia katika utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, afya, nishati ya umeme, kilimo na elimu.
Ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Japan unazingatia mwongozo wa Agenda ya Umoja wa Mataifa ya Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu inayojikita kwenye kupunguza umasikini na kukuza maendeleo. Japan ni miongoni mwa washirika wakubwa wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania kupitia JICA kuanzia mwaka 1962.
Tanzania ni nchi pekee inayoshirikiana na Japan katika maeneo matatu ya ushirikiano yaliyopewa kipaumbele na nchi hiyo ikiwemo, ushirikiano katika misaada na mikopo ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo; ujuzi na uzoefu kupitia program ya wajapani ya kujitolea chini ya Japan Overseas Cooperation Agreement; na fursa za mafunzo na masomo.






